VETA yadhamiria kuandaa vyema zana zake kwa msimu ujao SHIMMUTA
Timu za Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) zimeyaaga mashindano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA), kwa ushindani mkubwa, ijapokuwa nyingi zimekwama kufikia fainali na kutwaa ushindi.
Mashindano yamehitimishwa , tarehe 21 Novemba 2026, ambapo VETA imekataa kurudi mikono mitupu, ikakamata nafasi ya tatu katika mchezo wa bao, ambapo Mkufunzi wa Fani ya Ushonaji kutoka Chuo cha VETA cha Wilaya Pangani, Neema Likachi ndiye aliyeitoa VETA kimasomaso. Likachi ametunukiwa kombe la ushindi na Mhe. Dkt. Pius Chaya, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji aliyekuwa mgeni rasmi wa hafla ya ufungaji mashindano hayo kwenye viwanja vya Jamhuri, manispaa ya Morogoro.
Katika mashindano hayo VETA ilishiriki katika michezo saba, ikiwemo netiboli; mpira wa miguu; riadha; drafti; mbio za wazee wa miaka 50 na zaidi na kukimbia na gunia na pooltable.
Katika mchezo wa netiboli VETA iliishia 32 bora; mpira wa miguu 16 bora; riadha kwa wanaume mita 100 nafasi ya 5; mita 200 nafasi ya 4; mita 400 nafasi ya 4; kukimbia na gunia mita 100 nafasi ya 6; mbio za wazee umri wa miaka 50 na zaidi mita 800 nafasi ya 6; drafti kwa wanaume nafasi ya 4; mchezo wa drafti kwa wanawake nafasi ya 2 na na pooltable nafasi ya 5 hatua ya makundi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa VETA, baada ya kupokea kombe la ushindi wa mchezo wa bao, Mkuu wa Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC), Dkt Andrew Boi amewataka washiriki kuendelea na mazoezi wakati wote wanaporejea vituoni kwao badala ya kukaa na kusubiri wakati wa kushiriki michezo hiyo pekee.
Aidha ameshauri ofisi za Kanda za VETA kuwa sehemu ya kuandaa wachezaji ili kurahisisha upatiakanaji wa wachezaji wenye viwango watakaounda timu zenye kuleta ushindani na ushindi katika mashindano hayo.
Akizungumzia ushiriki kwa ujumla, Mwenyekiti wa Kamati ya VETA ya Michezo, Christopher Msigwa amesema timu zote zimepambana vikali na kwamba wao wakiwa ni mafundi wenye ujuzi hawana sababu za kulaumu vyombo vyao, bali ni kuandaa vyema zana zao kwa ajili ya msimu ujao, kwani kuvunjika kwa koleo si mwisho wa uhunzi.
Amesema licha ya kutotwaa ubingwa, mwaka huu ushiriki wa VETA umekuwa wa mafanikio makubwa, kwani tangu 2024 ilipoanza kushiriki, ni kwa mara ya kwanza timu za mpira wa miguu na netboli zimeingia 32 bora kati ya timu 96 zilizokuwa zikishiriki michezo hiyo na kwamba mwaka huu wamefanikiwa kushiriki michezo saba kati ya 12 ya mashindano hayo.
“Mkakati wetu ni kuanza kuandaa timu imara zaidi kwa ajili ya mashindano yajayo kwa kuanzia ngazi ya chuo, kanda na hatimaye kuunda timu bora ya VETA,” amesema.
Msigwa amesema miongoni mwa changamoto zinazochangia kutokufanya vizuri zaidi ni pamoja na kukosekaa kwa hamasa ya michezo katika ngazi zote za VETA kuanzia vyuo, kanda hadi Makao Makuu.
Ameshauri kuandaliwe sera au mwongozo kuhusu michezo ndani ya VETA na kuwa na utaratibu wa ligi ndogondogo katika ngazi za vyuo na kanda ili kusaidia kuwaandaa zaidi watumishi kimichezo.
