Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Chaya, akikabidhi kombe kwa Mkufunzi wa Fani ya Ushonaji kutoka Chuo cha Wilaya cha VETA Pangani, Neema Likachi, baada ya kuibuka mshindi wa tatu katika mchezo wa bao kwa wanawake kwenye Mashindano ya SHIMMUTA 2026, yaliyofanyika mkoani Morogoro.
Dkt. Andrew Boi akikabidhiwa kombe kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa VETA na Neema Likachi baada ya kuibuka mshindi wa tatu katika mchezo wa bao kwa wanawake. Makabidhiano hayo yamefanyika katika ukumbi mdogo wa mikutano wa MVTTC, Morogoro, Novemba 21, 2026.
………….
Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kimepata nafasi ya tatu katika mchezo wa bao kwa wanawake kupitia mshiriki wake Neema Likachi, Mkufunzi wa Fani ya Ushonaji kutoka Chuo cha Wilaya cha VETA Pangani, katika Mashindano ya SHIMMUTA 2026 yaliyofanyika mkoani Morogoro.
Likachi amekabidhiwa kombe na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Chaya, katika hafla ya kufunga mashindano hayo iliyofanyika Novemba 21, 2026, katika viwanja vya Jamhuri, Morogoro.
Katika mashindano hayo yaliyofanyika Novemba 6 hadi 21, VETA ilishiriki michezo mbalimbali ikiwemo netiboli, mpira wa miguu, riadha, bao, drafti na pool table.
Miongoni mwa matokeo yaliyopatikana ni nafasi ya pili katika drafti kwa wanawake, nafasi ya nne kwa wanaume katika drafti, pamoja na nafasi ya nne katika riadha ya mita 200 na 400. Timu za netiboli na mpira wa miguu zilifikia hatua ya 32 bora na 16 bora mtawalia.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Mkuu wa Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC), Dkt. Andrew Boi, amewapongeza wachezaji kwa ushiriki wao na kuwataka kuendelea kufanya mazoezi wanaporejea katika vituo vyao badala ya kusubiri mashindano yanapokaribia.
Aidha, amezishauri Ofisi za Kanda za VETA kushiriki katika kuibua na kuandaa vipaji vya michezo ili kujenga timu imara zitakazoshiriki kwa ushindani katika mashindano yajayo.
