Afisa manunuzi wa kampuni hiyo, Anirudh  Shekhawat akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Saalam.

……

Kampuni yajivunia fursa za kibiashara na wateja wapya iliyowapata kupitia maonesho ya madini.

Na Happy Lazaro, Dar es Salaam

Dar es Saalam.KAMPUNI ya Akshar Mining Services Limited imesema maonesho ya saba ya madini na uwekezaji yamekuwa fursa muhimu ya kukuza biashara zake, kutangaza huduma na kujenga mahusiano mapya na wadau wa sekta ya madini ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa manunuzi wa kampuni hiyo, Anirudh 

 Shekhawat amesema kampuni inajihusisha na maeneo makuu matatu ambayo ni uchimbaji wa madini kwa mikataba, uchimbaji wa visima na utafiti wa madini pamoja na usambazaji wa vifaa na mahitaji mbalimbali ya migodi.

Amesema kupitia huduma hizo, kampuni imekuwa ikifanya kazi na wadau mbalimbali wa sekta ya madini, wakiwemo Shanta Gold, Perseus Mining na Barrick, hatua inayodhihirisha ushiriki wake katika shughuli za uchimbaji na uzalishaji wa madini.

Anirudh amefafanua kampuni pia husambaza mahitaji mbalimbali ya migodi ikiwemo nyaya, vifaa vya kujikinga na usalama kazini (PPE), kemikali na vifaa vingine vinavyotumika katika shughuli za uchimbaji.

Anirudh amesema maonesho hayo yameiwezesha kampuni kukutana na wateja wapya, kujadiliana nao kuhusu fursa za biashara na kuweka msingi wa ushirikiano utakaochangia kupanua wigo wa shughuli zake katika siku zijazo.

Amesema wamepata pia nafasi ya kukutana na baadhi ya viongozi wa Serikali, wakiwemo mawaziri, ambao wamepongeza juhudi za kampuni kuingia katika sekta ya madini na kupanua huduma zake, jambo alilosema linaongeza hamasa ya kuendelea kuwekeza.

“Mafanikio na mipango ya ukuaji wa kampuni hiyo yanaungwa mkono na dira ya wakurugenzi wake, ambao wana malengo ya kuifanya Akshar Mining Services kuwa kampuni yenye wigo mpana zaidi wa huduma katika sekta ya madini.”amesema Anirudh.

Amesema kampuni ina matumaini ya kutumia fursa zilizopatikana katika maonesho hayo kuimarisha ushirikiano uliopo, kupata wateja zaidi na kuongeza mchango wake katika shughuli za uchimbaji na ugavi wa mahitaji ya migodi nchini Tanzania.