Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Bruno Sunguya, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof. Appolinary Kamuhabwa, pamoja na wadau wengine, wakishiriki katika matembezi ya hisani yaliyofanyika leo, Novemba 21, 2026, katika viwanja vya MUHAS, Dar es Salaam

………

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM

Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimewakutanisha washiriki zaidi ya 700, wakiwemo wahitimu, wanafunzi, wafanyakazi na wadau wa afya kutoka ndani na nje ya nchi, katika matembezi na mbio za hisani zilizolenga kuhamasisha jamii kufanya mazoezi mara kwa mara, kuzingatia lishe bora na kufuatilia afya zao ili kupunguza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza.

Akizungumza leo, Novemba 21, 2026, wakati wa matembezi na mbio za hisani iliyofanyika katika viwanja vya MUHAS, Dar es Salaam, mgeni rasmi, Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Bruno Sunguya, amepongeza uongozi wa chuo kwa kuandaa matembezi hayo, akieleza kuwa yamewakutanisha watu mbalimbali wenye uhusiano na taasisi hiyo, wakiwemo waliowahi kusoma na kufanya kazi chuoni hapo.

Prof. Sunguya amesema Serikali imekuwa ikihimiza wananchi kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora, akibainisha kuwa hatua hizo ni muhimu katika kuimarisha afya na kuzuia magonjwa.

Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa, amesema matembezi hayo yamefikia msimu wa tano tangu kuanzishwa kwake, huku chuo kikiendelea kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kujikinga na magonjwa kupitia mtindo bora wa maisha.

Prof. Kamuhabwa amesema katika matembezi hayo, pia wameshiriki wadau kutoka mataifa mbalimbali, yakiwemo Marekani, Sweden na Ujerumani, na kuahidi kuwa MUHAS itaendeleza utaratibu huo kutokana na kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza, ambayo yanaweza kupunguzwa kwa kufanya mazoezi na kuzingatia afya.

Baadhi ya washiriki wamepongeza MUHAS kwa kuanzisha programu hiyo, wakieleza kuwa imekuwa chachu ya kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za kimwili na kujenga mazoea ya kujali afya zao.

Katika matembezi na mbio hizo, washiriki walishindana katika umbali wa kilomita moja, tano, 10 na 15, huku washindi wa kila kundi wakikabidhiwa vyeti na mgeni rasmi, Prof. Sunguya.