Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi akisalimiana na mchambuzi wa masuala ya mazingira na tabianchi kutoka Norway Bw. Herald Frankie muda mfupi baada ya kuwasili katika banda la Jamhuri ya Malawi Novemba 12, 2026 kushikiri mkutano wa pembezoni uliojadili utekelezaji wa Ibara ya 6 ya Mkataba wa Paris wa mwaka 2015 ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya tabianchi unaoendelea katika Mji wa Antalya, Uturuki.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi akifurahia jambo na Makamu wa Rais wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (IATA), Marie Thomsen muda mfupi baada ya kuwasili katika banda la Jamhuri ya Malawi Novemba 12, 2026 kushikiri mkutano wa pembezoni uliojadili utekelezaji wa Ibara ya 6 ya Mkataba wa Paris wa mwaka 2015 Novemba 12, 2026 ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya tabianchi unaoendelea katika Mji wa Antalya, Uturuki.
……….
Serikali imetenga Shilingi Bilioni 6.6 ili kukiwezesha Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) kujenga uwezo wa kitaalamu na kuimarisha mifumo ya usajili wa miradi ya kaboni nchini.
Hayo yamebainishwa Novemba 12, 2026 na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi wakati wa mkutano wa viongozi na wataalamu wa Serikali na wadau wa maendeleo uliojadili utekelezaji wa Ibara ya Sita ya mkataba wa Paris wa mwaka 2015.
Mkutano huo umefanyika katika banda la Jamhuri ya Malawi pembezoni mwa mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya tabianchi unaoendelea katika Mji wa Antalya, Uturuki.
Dkt. Muyungi amesema fedha hizo zimekusudia katika kuimarisha uwezo wa wataalamu katika masuala ya upimaji, utoaji taarifa na uhakiki wa upunguzaji wa gesi joto sambamba na kuimarisha mfumo wa kitaifa wa usajili wa miradi ya kaboni.
Amefafanua kuwa Tanzania ni Nchi mwanachama wa itifaki ya kyoto ya mwaka 1997 na makubaliano ya paris ya mwaka 2015 ambayo inatoa utaratibu kwa nchi wanachama kupunguza gesijoto na kufaidika na biashara ya kaboni.
Amesema kupitia itifaki na mkataba huo, Tanzania imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya mapitio ya sera, uandaaji wa kanuni, mikakati na miongozo inayolenga kuweka utaratibu na masharti kwa wadau na wajasiriamali wa biashara ya kaboni.
Amefafanua kuwa kanuni na mwongozo wa usimamizi wa biashara ya Kaboni zimejikita katika kuimarisha mchango wa nchi katika jitihada za kupunguza uzalishaji wa gesijoto na ushiriki wa jamii, uwazi, ufanisi, ujumuishaji wa faida za kijamii na kiuchumi.
“Kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2025, Serikali imeanzisha Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) kama hatua muhimu ya kuweka utaratibu na mfumo wa usimamizi wa biashara ya kaboni” amesema Dkt. Muyungi.
Amesema hadi sasa NCMC imeweza kusajili zaidi ya miradi 100 ya biashara ya kaboni katika sekta mbalimbali ikiwemo misitu, nishati, kilimo, uchukuzi na udhibiti wa taka na pia Serikali imepanga kuongeza wigo wa vyanzo vipya vya biashara ya kaboni ikiwemo sekta ya usafirishaji.
Mkutano huo pia umeshirikisha viongozi na watalaamu wa masuala ya tabianchi akiwemo Waziri wa Maliasili na mabadiliko ya tabianchi wa Malawi, Mhe. Patricia Wiskies na wawakilishi kutoka Serikali za Eithiopia, Burkina Faso, Sweden, Norway na Chile.
Tanzania inatumia fursa ya mkutano wa COP 31 kuimarisha diplomasia ya kimataifa ya mabadiliko ya tabianchi, kutafuta fursa za fedha, utafiti, teknolojia na kujenga uwezo kwa wataalamu.
Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa COP 31 unaoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kaulimbiu ya kitaifa ya mkutano huo inasema “Hatua jumuishi za Tanzania za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa ajili ya dira 2050: Kujenga Taifa Imara la Kijani na lenye ustawi”.

