Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akihutubia viongozi mbalimbali katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali (Antalya Leaders’ Summit) kuhusu mabadiliko ya Tabianchi (COP31). Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa ANFAŞ Antalya Expo Center nchini Uturuki, tarehe 11 Novemba, 2026.

.………

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito wa kuwepo kwa mifumo ya uwazi katika soko la hewa ukaa itakayohakikisha bei ya hewa ukaa inakuwa ya haki, manufaa yanagawanywa kwa usawa na mazingira yanalindwa.

Akihutubia Mkutano wa 31 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) unaofanyika Antalya, Uturuki, Novemba 11, 2026, Rais Samia amesema utekelezaji wa Kifungu cha Sita cha Makubaliano ya Paris unapaswa kuhakikisha mifumo ya biashara ya hewa ukaa inazingatia misingi hiyo.

Amesema mifumo hiyo inapaswa kuwa na uwazi katika upangaji wa bei, mgawanyo wa manufaa na kulinda uadilifu wa kimazingira, huku ikisaidia kuongeza rasilimali kwa ajili ya jamii za maeneo husika na maendeleo ya taifa.

Rais Samia ameeleza kuwa Tanzania ina fursa mbalimbali za hewa ukaa katika sekta za usafiri, usimamizi wa taka na uzalishaji wa nishati jadidifu ikiwemo umeme wa maji, jotoardhi na upepo.

Ameongeza kuwa rasilimali za misitu ni sehemu muhimu ya fursa hizo, akibainisha kuwa Tanzania ina misitu yenye ukubwa wa takribani hekta milioni 48.1.

Amesema fursa hizo zinapaswa kuendelezwa kupitia mifumo inayozingatia uwazi na haki ili kuhakikisha manufaa ya rasilimali za hewa ukaa yanachangia maendeleo ya nchi na jamii zinazohusika.