Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb), amesema Tanzania itaendelea kuimarisha misingi ya Umoja wa Afrika, usalama wa pamoja na ushirikiano wa kikanda kwa lengo la kudumisha amani na usalama barani Afrika.

Dkt. Nyansaho ameyasema hayo Novemba 11, 2026, jijini Arusha, wakati akifunga rasmi Mkutano wa 20 wa Makamanda wa Vyuo vya Ukamanda na Mafunzo ya Kijeshi barani Afrika (African Conference of Commandants – ACoC).

Katika hotuba yake, Waziri huyo aliwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa washiriki wote wa mkutano huo.

Aidha, aliwapongeza makamanda na wajumbe kwa ushiriki wao na michango yenye tija katika kuimarisha elimu ya kijeshi na kukuza ushirikiano baina ya taasisi za kijeshi barani Afrika.

Alieleza kuwa elimu na mafunzo ya kitaaluma ya kijeshi yana nafasi muhimu katika kuandaa viongozi wenye maarifa, maono na uwezo wa kukabiliana na changamoto za kiusalama zinazolikabili bara la Afrika, zikiwemo ugaidi, uhalifu wa kupangwa unaovuka mipaka ya nchi na vitisho vya kimtandao.

Pia, alihimiza kuimarishwa kwa ushirikiano baina ya vyuo vya kijeshi kupitia mafunzo ya pamoja, kubadilishana wanafunzi na wakufunzi pamoja na kuoanisha mitaala ya mafunzo, hususan katika maeneo ya Operesheni za Kusaidia Amani, Sheria za Kimataifa za Kibinadamu na Ulinzi wa Raia.

Mkutano huo uliwakutanisha viongozi waandamizi wa kijeshi na wajumbe kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, akiwemo Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Salumu Haji Othman, Mkuu wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa ACoC, Meja Jenerali Stephen Justice Mnkande, pamoja na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Mabele.

Wengine ni wawakilishi wa Umoja wa Afrika, makamanda wa vyuo vya kijeshi, wakufunzi wakuu na maafisa waandamizi wa kijeshi.

Mkutano huo umekuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu bora za mafunzo ya kijeshi, kwa lengo la kuimarisha uwezo wa pamoja wa majeshi ya Afrika na kukuza ushirikiano katika kukabiliana na changamoto za kiusalama, hatua inayochangia juhudi za kudumisha amani, usalama na utulivu wa kudumu barani Afrika.