NA DENIS MLOWE

MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Cosato Chumi, ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Youth Investors Association (YIA), taasisi inayojikita katika kuhamasisha uwekezaji, ujasiriamali na kuwawezesha vijana kiuchumi.

Uteuzi huo unamweka Chumi katika nafasi ya kushauri na kuunga mkono ajenda za taasisi hiyo zinazolenga kuwafungulia vijana fursa za uwekezaji, kukuza ubunifu, kuendeleza ujuzi na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za maendeleo.

Chumi ana uzoefu wa utumishi wa umma na uongozi, akiwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini kwa kipindi cha mwaka 2015 hadi 2025, kabla ya kuingia katika Bunge la Afrika Mashariki, ambako anawakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika kipindi cha utumishi wake bungeni, pia aliwahi kushika nafasi ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuanzia mwaka 2024 hadi 2025, pamoja na kuwa mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Kabla ya kuingia bungeni, Chumi alihudumu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kama Afisa wa Diplomasia kuanzia mwaka 2007 hadi 2015, huku awali akifanya kazi katika Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuanzia mwaka 2002 hadi 2006.

Katika maelezo ya YIA kuhusu mwenyekiti Chumi meelezwa kuwa ana shauku kubwa katika masuala ya uwezeshaji vijana, fursa za uwekezaji na nafasi ya vijana katika kuunda mustakabali wa maendeleo.

Chumi anaamini vijana si viongozi wa baadaye pekee, bali ni washirika muhimu katika kusukuma maendeleo ya sasa, akihimiza kuwepo kwa mazingira yatakayowawezesha kupata fursa za uwekezaji, msaada wa ujasiriamali, mafunzo ya ujuzi, ubunifu na kushiriki katika maamuzi.

Aidha, anatarajiwa kuunga mkono mipango inayolenga kufungua uwezo wa vijana, kuwaunganisha na fursa mpya za kiuchumi na kuwawezesha kuwa sehemu muhimu ya mageuzi ya maendeleo ya kitaifa na kikanda.