Na Genofeva Matemu – Dar es Salaam

21/11/2026

Tanzania na Malawi zimefikia makubaliano ya kuanzisha mpango wa rufaa za wagonjwa utakaoiwezesha Malawi kuleta wagonjwa wanaohitaji huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi yakiwemo matibabu ya moyo nchini Tanzania.

Makubaliano hayo yanayotarajiwa kuzaa mkataba rasmi wa ushirikiano yamelenga kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili katika sekta ya afya, kupunguza gharama za matibabu na kuongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa ambazo bado hazipatikani nchini Malawi.

Akizungumza jana wakati wa kikao cha viongozi kutoka sekta za afya kati ya nchi hizo mbili Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia vifaa tiba na dawa Emmanuel Tayari alisema Tanzania imeendelea katika kutoa huduma bingwa bobezi ikiwemo huduma za matibabu ya moyo, saratani, mifupa na huduma nyingine za kibingwa ambazo bado zinaendelea kuimarishwa nchini Malawi.

Emmanuel alisema ushirikiano wa Tanzania na Malawi hautaishia katika rufaa za wagonjwa pekee bali utatoa fursa kwa wataalamu wa afya wa Malawi kupata mafunzo nchini Tanzania, kufanya tafiti za pamoja na kubadilishana uzoefu wa kitaalamu, hatua itakayochangia kuimarisha mfumo wa huduma za afya kati ya nchi hizo mbili.

“Tutabainisha hospitali zitakazopokea wagonjwa wanaotoka nchini Malawi pamoja na kuhakikisha kuwa hospitali hizo zinatunza kumbukumbu sahihi za matibabu na gharama za huduma zinazotolewa kwa wagonjwa watakaotumwa kupitia mpango huu”, alisema Emmanuel

Kwa upande wake Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Afya nchini Malawi Dkt. Dan Namalika alisema Serikali ya Malawi imeahidi kurahisisha upatikanaji wa viza kwa wagonjwa watakaokuja nchini Tanzania kwaajili ya kupata huduma za matibabu na kuhakikisha malipo ya gharama za matibabu yanafanyika ndani ya siku 90 baada ya kuwasilishwa kwa ankara za huduma zilizokubaliwa.

Dkt. Namalika alisema ushirikiano huo ni hatua muhimu itakayobadilisha mfumo wa sasa wa Serikali ya Malawi kugharamia mamilioni ya dola kila mwaka kupeleka wagonjwa katika nchi za mbali kama Afrika Kusini na India kwa ajili ya kupata huduma za matibabu ya kibingwa yakiwemo magonjwa ya moyo.

“Kupitia mpango huu Malawi inatarajia kupunguza gharama za matibabu na usafiri, muda wa safari pamoja na kuwawezesha wagonjwa kupata huduma za kibingwa katika nchi jirani ya Tanzania”, alisema Dkt. Namalika

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema wataalam kutoka nchini Malawi wametembelea Taasisi hiyo na kuvutiwa na miundombinu, huduma na mazingira ya hospitali.

“Tumewaonesha miundombinu tuliyoiwekeza katika Taasisi yetu ikiwemo mashine za kisasa zinazotumia akili unde, wataalamu hao wamevutiwa na huduma zetu na kuipongeza Serikali ya Tanzania kwa uwekezaji mkubwa walioufanya”, alisema Dkt. Angela

Nchi hizo zimekubaliana kushirikiana katika masuala ya ulinzi wa taarifa za wagonjwa, mafunzo ya wataalamu wa afya, tafiti za kisayansi na kubadilishana ujuzi na uzoefu wa kitaalamu.