Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally chirukile (katikati), Mkurugenzi wa taasisi ya COCO Doreen Simpungwa (kushoto wa kwanza) wakati wa hafla ya kupokea matundu 10 ya vyoo katika shule ya sekondari Itwelele iliyopo manispaa ya Sumbawanga.

…………..
Na Neema Mtuka, Sumbawanga
Rukwa.Shirika la Community for Change Organization (COCO) limekabidhi rasmi matundu 10 ya vyoo yenye thamani ya shilingi million 46 kwa Shule ya Sekondari Itwelele iliyopo Manispaa ya Sumbawanga, Mkoani Rukwa.
Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika leo 18,Novemba ,2026 shuleni hapo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, walimu na wanafunzi.
Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Mhe. Nyakia Ally Chirukile, ambaye ndiye aliyepokea vyoo hivyo kwa niaba ya Serikali.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya amesema Serikali ina thamini sana mchango wa wadau kama COCO katika kuboresha miundombinu ya elimu.
“Tunawashukuru COCO kwa kazi kubwa mnayofanya vyoo hivi vitasaidia sana kuboresha afya, usafi na heshima kwa wanafunzi wetu, hasa watoto wa kike.
Serikali haiwezi peke yake, tunahitaji wadau kama hawa,” amesema Mhe. Chirukile.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Community for Change Organization (COCO), Doreen James Simpungwe, amesema shirika lao wakishirikiana na Rukwa Foundation waliamua kujenga vyoo hivyo baada ya kuona changamoto kubwa ya upungufu wa vyoo shuleni hapo.
“Tuliona wanafunzi wanapata tabu sana ndiyo maana tukaamua kujenga matundu 10 ya kisasa yenye thamani ya mill 46 ili wanafunzi wasome katika mazingira safi na salama,” amesema Doreen Simpungwe.
Ameongeza kuwa COCO itaendelea kushirikiana na Serikali na jamii katika kuboresha elimu, afya na ustawi wa watoto na vijana mkoani Rukwa.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Itwelele, Peter M. Mwakasege, ameishukuru COCO kwa niaba ya walimu na wanafunzi, akisema vyoo hivyo vitapunguza msongamano na kuongeza ufaulu.
“Kwa niaba ya walimu na wanafunzi, tunashukuru sana hii ni zawadi kubwa kwa shule yetu sasa wanafunzi wetu watakuwa na mazingira bora ya kujifunzia,” amesema Mwalimu Mwakasege.
Nao baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo akiwemo Daniel Mipata amewataka wadau wengine kujitokeza kuwachangia ujenzi wa bweni la wavulana.
Huku Sara Ayubu mwanafunzi wa kidato cha tatu akionesha furaha na kusema kuwa sasa wana uhakika wa usafi na faragha wakiwa shuleni.
