*Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuongoza zoezi la kuhudumia wananchi
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imewataka wananchi wa Mkoa wa Arusha na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki uzinduzi wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria pamoja na Kliniki ya Sheria bila malipo itakayofanyika kuanzia Novemba 23 hadi 29, 2026 katika Viwanja vya Sanawari Mataa jijini Arusha.
Wito huo umetolewa na Wakili wa Serikali wa Mkoa wa Arusha, kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bi. Veritas Mlay, leo Jumatano Novemba 18, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, akieleza kuwa uzinduzi rasmi wa Kamati hiyo utafanyika Novemba 24, mwaka huu.
Amesema Mkoa wa Arusha umepata bahati ya pekee kwani zoezi la utoaji wa ushauri wa kisheria litaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Saidi Johari, ambaye pia atakuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo.
Ameeleza kuwa kliniki hiyo itahusisha wataalamu zaidi ya 50, wakiwemo Mawakili wa Serikali, wataalamu wa ardhi na ustawi wa jamii, watakaotoa ushauri kuhusu masuala ya ardhi, mirathi, ajira, ndoa na familia, biashara, haki za binadamu pamoja na changamoto nyingine za kisheria.
Bi. Mlay amesema Kamati za Ushauri wa Kisheria zimeanzishwa kwa lengo la kusogeza huduma za kisheria karibu na wananchi, kutoa elimu ya sheria, kupunguza malalamiko na migogoro dhidi ya Serikali pamoja na kusaidia kukabiliana na vitendo vya uonevu na ukiukwaji wa sheria.
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imewahimiza wananchi kutumia fursa hiyo kuwasilisha changamoto zao na kupata ushauri kutoka kwa wataalamu bila gharama yoyote, akisisitiza kuwa huduma hizo zitapatikana kwa siku saba kuanzia Novemba 23 hadi 29, 2026.
