Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Novemba 18, 2026
WAKURUGENZI wa Halmashauri mkoani Pwani wameagizwa kuhakikisha Dashibodi ya Ramani ya Hatari za Tabianchi inayotumika katika sekta ya elimu inafanya kazi kikamilifu ili kutambua mapema vihatarishi vinavyoweza kuathiri shule na kuchukua hatua za kukabiliana navyo.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, katika uzinduzi wa dashibodi hiyo inayolenga kusaidia kubaini shule zilizo katika hatari ya kukumbwa na mafuriko na ukame, pamoja na kutoa tahadhari za haraka kupitia ujumbe mfupi wa simu (SMS).
Nyongo amesisitiza kuwa uzinduzi wa mfumo huo haupaswi kuwa tukio la kawaida lisilo na matokeo, bali unapaswa kuambatana na matumizi endelevu yatakayosaidia kutatua changamoto zilizokusudiwa na kuhakikisha wanafunzi wanaendelea kupata elimu katika mazingira salama licha ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ameelekeza wakuu wa shule kutumia taarifa zinazopatikana kwenye mfumo kutambua vihatarishi katika maeneo yao na kuandaa mipango ya kukabiliana na majanga kulingana na mazingira ya shule husika.
Aidha, maofisa elimu wa kata na wilaya wametakiwa kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa matumizi yake ili taarifa hizo zijumuishwe katika mipango ya kuimarisha usalama wa shule.
Pia, ameutaka mkoa na maofisa elimu kushirikiana na maofisa TEHAMA wa mkoa na halmashauri kutoa msaada wa kitaalamu na kutatua kwa haraka changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa matumizi ya mfumo huo.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Timu ya Programu ya Shule Bora, Virginia Briand, amesema kuboresha ubora wa elimu kunahitaji miundombinu himilivu, walimu wenye uwezo, mazingira salama ya kujifunzia na mifumo imara inayowezesha shule kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema katika kipindi cha miaka sita ya utekelezaji wa programu hiyo, imefanikiwa kusaidia kuweka teknolojia za kupikia safi katika shule 22 za mikoa ya Pwani na Katavi, zikiwemo 12 za Pwani, pamoja na kukamilika kwa takribani madarasa 121 yanayozingatia ustahimilivu dhidi ya athari za tabianchi katika shule 80, zikiwemo shule 10 za Pwani.
Ameongeza kuwa Programu ya Shule Bora inayofadhiliwa na Serikali ya Uingereza kupitia FCDO, inatekelezwa chini ya Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kwa msaada wa kitaalamu wa Cambridge Education.
Naye mwakilishi wa Mkurugenzi wa TEHAMA wa Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI, Erick Lesilwa, amesema dashibodi hiyo ni nyenzo muhimu ya kuboresha utendaji na kuhakikisha kila mtoto anapata elimu katika mazingira salama.

