*Rais Samia achangia milioni 200, asifu mchango wa taasisi za dini katika maendeleo ya taifa.

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amefanikisha kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 1.547 katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Ofisi za Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Mkoa wa Tabora.

Harambee hiyo imefanyika leo (Jumanne, Novemba 17, 2026) katika ukumbi wa Muungano, Mkoani Tabora, ambapo ameipongeza BAKWATA kwa maono ya ujenzi wa Ofisi hiyo.

Akizungumza katika harambee hiyo, Dkt. Mwigulu amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye katika harambee hiyo amechangia shilingi milioni 200, anaunga mkono jitihada zinazofanywa na madhehebu ya dini na anathamini mchango wao katika ustawi wa taifa.

Amesema kuwa Rais Dkt. Samia anatambua kuwa taasisi za dini zimekuwa mshirika muhimu wa serikali katika malezi, kuimarisha maadili katika jamii na utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo afya na elimu.

Dkt. Mwigulu amesema kuwa mchango huo umeifanya Tanzania kuendelea kuwa mfano wa amani barani Afrika na duniani kote. “Palipo na mshikamano, umoja, utulivu, amani na uzalendo, ni dhahiri nchi inaweza kupiga hatua, na wananchi wake wanaweza kupiga hatua”.

Amesema kuwa kwa zaidi ya nusu karne, BAKWATA imeendelea kuwa taasisi muhimu katika ujenzi wa taifa mbali na jukumu lake la msingi la mafundisho ya kidini. “BAKWATA imeendelea kuwa mshirika wa karibu wa masuala ya msingi nchini, hasa kwa kuzingatia maadili, uzalendo, na mshikamano”

Amesisitiza kuwa maendeleo ya taifa lolote hayapimwi tu kwa kila mmoja kuwa na maendeleo yake binafsi au miundombinu pekee, lakini yanapimwa pia kwa kiwango cha maadili, mshikamano uliopo katika taifa husika.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia amenituma niwahakikishie kuwa serikali anayoiongoza itaendelea kuheshimu na kuenzi mshikamano kati ya Serikali na taasisi zetu za dini,” amesisitiza Dkt. Mwigulu.

Akisoma taarifa ya Mradi wa ujenzi wa Ofisi hiyo, Katibu wa Bakwata mkoa wa Tabora, Mohamed Hussein Abeid amesema kuwa ofisi hiyo ambayo itakuwa na ghorofa tano pindi itakapokamilika litagharimu shilingi bilioni 1.8.

“Jengo hili litakapokamilika litakuwa na Ofisi za Baraza na Taasisi zake, maduka ya biashara, Ofisi za kupangisha kwa taasisi mbalimbali, ukumbi wa mikutano, sehemu ya kupumzikia kwa ajili ya viongozi wakuu wa baraza na wageni wengine, ujenzi wa jengo hili unategemea kukamilika ndani ya miezi 18”