Baadhi ya vijana kutoka mashirika mbalimbali wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi

Katibu Tawala wa Wilaya ya Nyamagana Thomas Salala akizungumza kwenye warsha iliyofanyika katika ukumbi wa Nyakahoja Jijini Mwanza.

Mkurugenzi wa Shirika la Power of Youth Development Pedius Boniphace akizungumza kwenye warsha ya siku moja iliyowakutanisha vijana na viongozi wa fursa za vijana Jijini Mwanza

…………

Na Hellen Mtereko, Mwanza

Vijana wametakiwa kutafuta taarifa sahihi kupitia vyanzo rasmi kuhusu fursa mbalimbali zilizopo nchini ili waweze kunufaika nazo.

Rai hiyo imetolewa Novemba 13, 2026 na Afisa Maendeleo ya Vijana kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Michael Magesa wakati alipokuwa akizungumza na vijana kutoka mashirika mbalimbali ambao wameshiriki kwenye warsha ya siku moja iliyoandaliwa na shirika la Power of Youth Development (PYD).

Amesema vijana wengi hutegemea taarifa za kusikia ambazo mara nyingi si sahihi hatua inayopelekea kushindwa kupata fursa na uwezeshwaji kikamilifu.

“Vijana mnakosa fursa kwasababu hamtafuti taarifa za wapi fursa zilipo,na kama haupati taarifa huwezi kupata fursa sahihi hivyo niwaombe sana muwe wepesi katika kutafuta taarifa ili mnufaike na fursa za uwezeshaji zinazotolewa na Serikali”, Amesema Magesa

Akizungumzia suala la mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri amesema mikopo hiyo haiombwi kwa maandiko mradi yaliyopo kwenye makaratasi bali inaombwa kwenye mfumo na majibu yanapatika kwenye mfumo hivyo amewasihi vijana kufuata maelekezo na utaratibu ili wapate mikopo na fursa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Power of Youth Development (PYD) Pedius Boniphace amesema waliandaa warsha hiyo ili vijana zaidi ya 40 kutoka mashirika mbalimbali waweze kukutana na taasisi zinazosimamia na kutekeleza fursa za kisera za vijana ili wajadili fursa za kiuchumi zinazopatikana hususani suala la mitaji.

Alieleza kuwa Warsha hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi ambao unatekelezwa na UNDP kwakushirikiana na Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana ambao unaitwa ‘Dumisha amani’

“Huu ni mradi unaotekelezwa kwaajili ya kuwawezesha vijana kuendelea kudumisha amani”, Alisema Boniphace

Amesema walikutana na vijana hao miezi mitano iliyopita wakazungumza nao ambapo wengi wao walionesha kutokuwa na imani na taasisi za umma zinazosimamia fursa zao.

Baada ya kuona vijana hawana imani wakaona wawakutanishe na viongozi wanaosimamia hizo fursa ili wawaeleze vijana namna bora ya kuweza kufanya na hatimaye wazifikie fursa zinazowezeshwa na serikali.

Aidha, amesema Serikali inapaswa iwe inatoa taarifa kuanzia ngazi ya mtaa hatua itakayosaidia kupunguza malalamiko ya vijana ya kutofikiwa na fursa wanazozitoa sanjari na kuongeza bajeti kwani vikundi vinavyohitaji fedha za mikopo ni vingi.

Naye Afisa Uchunguzi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza, Magesa Cosmas ametoa wito kwa viongozi wanaohusika na utoaji wa mikopo kuhakikisha wanafuata sheria,kanuni na taratibu zilizoweka katika utoaji wa mikopo hiyo ili waweze kujiepusha na rushwa.

Akizungumza kwa niaba ya vijana walioshiriki kwenye warsha hiyo, Paul Kashilimu alisema wamekuwa wakikosa fursa mbalimbali kutokana na kukosa uelewa na kukosa mtandao wa wahusika wanaosimamia.

Amesema warsha hiyo imekuwa chachu kwake ya kuongeza jitihada katika kutafuta taarifa sahihi huku akiwapongeza viongozi wanaosimamia fursa zao kwa namna walivyo wapa mwanga mzuri wakuzifikia fursa.

Awali akizungumza kwenye warsha hiyo Katibu Tawala Wilaya ya Nyamagana ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya uhakiki wa fedha za mikopo zinazotolewa na Halmashauri, Thomas Salala aliwasisitiza vijana kuziheshimu na kuziogopa fedha za mikopo.

“Mnapochukua fedha hizi za mikopo hakikisheni mnazifanyia kazi ipasavyo na, lakini mkizibadilishia matumizi kwa tamaa hamtaweza kufanikiwa na mtashindwa kurejesha fedha hivyo kuweni na nidhamu kwenye suala la fedha”, Amesema Salala