Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka kipaumbele katika kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu, kwa kutambua mchango wake katika kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 14 Novemba 2026, alipofungua Kituo cha Elimu ya Anga cha Zanzibar Astronomy and Space Society (ZASS) na kuzindua rasmi Mradi wa Zanzibar Observatory and Planetarium, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema maendeleo ya taifa yanategemea uwekezaji katika maarifa, tafiti na teknolojia, hivyo Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya TEHAMA, tafiti na vituo vya teknolojia ili kuwajengea wananchi uwezo wa kushiriki kikamilifu katika uchumi wa maarifa.
Rais Dkt. Mwinyi amesema mradi huo utaongeza fursa kwa vijana kuibua vipaji, kukuza ubunifu na kujifunza kwa vitendo masomo ya sayansi, hususan elimu ya anga, sambamba na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030 na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050.
Amezitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu kushirikiana na ZASS katika kupanua elimu ya sayansi ya anga na kuwafikia wanafunzi wengi zaidi.
Akizungumzia historia ya Zanzibar katika sayansi ya anga, Rais Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar ina nafasi ya kipekee kutokana na kushiriki katika Mradi wa Mercury wa Shirika la Anga la Marekani (NASA), ambapo vituo vya mawasiliano na ufuatiliaji wa vyombo vya anga vilianzishwa katika maeneo ya Tunguu na Chwaka.
Kutokana na historia hiyo, ameitaka ZASS kwa kushirikiana na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kuangalia uwezekano wa kuanzisha Kituo Maalumu cha Maonesho kitakachohifadhi picha, nyaraka, ramani za kidijitali na kumbukumbu nyingine zinazohusu Mradi wa Mercury na mchango wa Zanzibar katika historia ya sayansi ya anga.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuhifadhi urithi wa kihistoria, kuongeza uelewa wa wananchi na kuwahamasisha vijana kupenda masomo ya sayansi.
Dkt. Mwinyi pia amewapongeza vijana walioshiriki katika maonesho ya ubunifu wa kisayansi, akiwataka kuendelea kujifunza, kufanya tafiti na kubuni teknolojia zitakazotoa suluhisho kwa changamoto za jamii na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amekubali ombi la kuwa Mlezi wa Zanzibar Astronomy and Space Society (ZASS), kutokana na kutambua mchango wa taasisi hiyo katika kukuza sayansi na elimu ya anga nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Mhe. Dkt. Mohammed Ali Suleiman, amesema kituo hicho kitaongeza fursa za elimu kwa vijana na matumizi ya teknolojia ya anga katika usimamizi wa mazingira, ufuatiliaji wa mabadiliko ya tabianchi, mawasiliano na Uchumi wa Buluu.
Amesema pia kitafungua fursa za ajira, ujasiriamali na tafiti katika TEHAMA, uchambuzi wa takwimu na utengenezaji wa programu za kompyuta.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa ZASS, Amina Ahmada, amesema mradi huo unatarajiwa kuipa Zanzibar nafasi mpya katika sayansi na teknolojia ya anga kupitia kituo cha uchunguzi wa anga, ukumbi wa kidijitali wa maonesho na programu za elimu ya anga.
Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi ametembelea mabanda ya wanafunzi kutoka skuli mbalimbali za Zanzibar na kupata maelezo kuhusu ubunifu wao katika masuala ya anga, sayansi na teknolojia, pamoja na kukata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa kituo hicho.

