Happy Lazaro, Arusha.
Arusha .Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Shirika la World Vision Tanzania zimesaini mkataba wa ushirikiano utakaolenga kuimarisha mifumo ya kuzuia rushwa, kuongeza uwazi na uwajibikaji pamoja na kuziba mianya ya vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kibinadamu.
Aidha hafla hiyo ya utiaji saini mkataba huo imefanyika katika makao makuu ya World Vision Tanzania jijini Arusha.
Akizungumza katika hafla hiyo , Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, amesema makubaliano hayo yataweka mfumo rasmi wa ushirikiano katika kuzuia, kubaini mianya ya rushwa na kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivyo.
Chalamila amesema ushirikiano huo utajikita katika maeneo mawili makuu ambayo ni kutoa elimu na kujenga uwezo kwa wadau kuhusu madhara ya rushwa pamoja na kuimarisha mifumo ya ndani ya udhibiti wa vitendo hivyo katika shughuli za World Vision Tanzania.
“Taasisi hizo zitashirikiana kuandaa mafunzo, semina, warsha na vipindi vya uhamasishaji kwa watumishi, viongozi, washirika, wazabuni na wanufaika wa miradi ili kuwajengea uelewa kuhusu viashiria vya rushwa, athari zake za kisheria, maadili na namna ya kutoa taarifa za vitendo hivyo.”amesema Chalamila.
Katika eneo la udhibiti, amesema watafanya tathmini ya viatarishi vya rushwa katika usimamizi wa fedha, manunuzi, mikataba na shughuli nyingine za kiutendaji, huku TAKUKURU ikitoa ushauri wa kitaalamu kuhusu mifumo ya udhibiti wa ndani na namna ya kudhibiti migongano ya maslahi.
Chalamila amesema mapambano dhidi ya rushwa hayawezi kufanikiwa kwa juhudi za taasisi moja pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta binafsi, vyombo vya habari na wananchi kwa ujumla.
Aidha, amesisitiza kuwa ushirikiano huo unaendana na Mkakati wa Taifa wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Mpango wa Utekelezaji wa Awamu ya Nne, unaohimiza ushiriki wa wadau wote katika mapambano dhidi ya rushwa.
Chalamila ametoa wito kwa waandishi wa habari kutumia nafasi zao kuelimisha jamii, kuibua vitendo vya rushwa na kutoa taarifa sahihi kwa TAKUKURU bila woga wala upendeleo, akieleza kuwa rushwa inakiuka haki za wananchi, inadhoofisha utawala bora, inakwamisha fursa za kiuchumi na kusababisha upotevu wa mapato ya Serikali.
Amesema kila Mtanzania ana wajibu wa kuwa sehemu ya suluhisho katika mapambano hayo ili kujenga taifa lenye misingi ya haki, uwazi, uadilifu na uwajibikaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa World Vision Tanzania, James Anditi, amesema safari ya kuanzisha ushirikiano huo ilianza Aprili 29, 2026, baada ya shirika hilo kufanya mazungumzo na TAKUKURU kuhusu uwezekano wa kuweka mfumo rasmi wa kushirikiana katika masuala ya kuzuia na kupambana na rushwa.
Anditi amesema uamuzi wa kuingia katika makubaliano hayo unaonesha dhamira ya World Vision Tanzania ya kuimarisha uwazi, uadilifu na uwajibikaji katika utekelezaji wa shughuli zake, huku akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa kushirikiana na taasisi za Serikali katika kulinda rasilimali na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa kuzingatia misingi ya uadilifu.

