Ahoji  uuzaji wa mali zenye thamani kubwa kwa madeni madogo

Asisitiza mkandarasi wa Itoni–Lusitu kurejea kazini Novemba 17

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka wataalamu wa sheria kuangalia mianya inayoweza kutumiwa vibaya katika minada ya mali za wananchi, hususan mali zenye thamani kubwa zinapouzwa kwa madeni madogo au salio dogo la mkopo.

Amesema amepokea malalamiko ya aina hiyo katika maeneo mbalimbali, yakiwemo ya wakopaji waliolipa sehemu kubwa ya mikopo lakini wanakabiliwa na kuuziwa mali zao zote.

“Kama kuna maeneo tumeweka loopholes za kisheria, lazima tuziangalie,” amesema.

Dkt. Mwigulu ametoa maelekezo hayo leo (Ijumaa, Novemba 13, 2026), wakati akizungumza na kusikiliza kero za wananchi katika mkutano wa hadhara mjini Ludewa, mkoani Njombe.

Kauli hiyo imefuatia malalamiko ya mwananchi kuhusu nyumba yake kuwekewa mnada kutokana na deni la shilingi milioni 1.2. Mthamini wa Halmashauri amesema nyumba hiyo ambayo haijakamilika ilithaminiwa kwa shilingi milioni sita.

“Mnauza nyumba ya milioni sita kulipa deni la milioni moja na laki mbili?” amehoji Waziri Mkuu.

Ametaka pia kuangaliwa kwa gharama zinazotozwa na madalali na ameahidi kumlipia mwananchi huyo deni la shilingi milioni 1.2.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amesisitiza mkandarasi wa barabara ya Itoni–Lusitu kurejesha mitambo na kuendelea na ujenzi ifikapo Novemba 17, 2026, baada ya Serikali kulipa madai yake.

“Wananchi hawa wala hawataki kuona magreda na mitambo. Wanataka kuona kazi ikiendelea,” amesema.

Pia, ameitaka Wizara ya Ujenzi kukamilisha maandalizi ya kitaalamu ya barabara inayounganisha sehemu iliyojengwa kwa zege na makao makuu ya Ludewa hadi maeneo ya miradi ya kiuchumi, ili ipewe kipaumbele Serikali itakapoanza kupokea miradi mipya.

Kuhusu mahindi, amesema Serikali imeielekeza Wizara ya Kilimo kuharakisha mauzo ya mazao yaliyopo, ikiwemo nje ya nchi, ili kuongeza nafasi ya kununua zaidi kutoka kwa wakulima. Pia, amesema Watanzania wanaohitaji kuuza mazao katika nchi jirani waruhusiwe kufanya hivyo.

Akisikiliza kero za ardhi, Waziri Mkuu ameagiza Ludewa ipangiwe Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya, baada ya kuelezwa kuwa baraza hilo linahudumiwa na mwenyekiti aliyepo Njombe.

Katika mkutano huo, Dkt. Mwigulu amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani aliyompa, akisema ametimiza mwaka mmoja tangu alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu Novemba 13, 2025.

“Hakuna kero iliyo ndogo. Kama inakukera, ni kero tu,” amesema.