Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, akizungumza kwenye kikao hicho jijini Arusha leo

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mhe. Paul Christian Makonda.

………..

Na Happy Lazaro, Arusha.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, ameitaka mikoa na halmashauri kuanza kuweka mikakati ya kuhakikisha miundombinu inayojengwa kwa ajili ya AFCON 2027 inakuwa chachu ya maendeleo ya michezo, ikiwemo kuifanya Arusha kuwa mwenyeji wa timu itakayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania.

Makalla amesema uwekezaji unaofanyika katika ujenzi na uboreshaji wa viwanja zaidi ya vitano unapaswa kuleta manufaa ya muda mrefu kwa wakazi wa Arusha, badala ya kutumika kwa kipindi cha mashindano pekee.

Amesema uwepo wa viwanja hivyo unatoa nafasi kwa mkoa kukuza utalii wa michezo, kuvutia mashindano mbalimbali na kuinua kiwango cha soka, hivyo ni muhimu kuhakikisha Arusha inakuwa na timu inayoweza kushindana katika Ligi Kuu.

Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) jijini Arusha, Makalla pia ameelekeza nguvu zaidi katika kuboresha elimu, akitaka ushirikiano wa wazazi, walezi, walimu na Serikali uwe sehemu ya mikakati ya kuongeza ufaulu.

Amebainisha kuwa baadhi ya shule zinazofanya vibaya zipo katika maeneo ya wafugaji, ambako kuhama kwa familia kufuata malisho ya mifugo kunachangia kukatiza masomo ya watoto, hali inayohitaji mikakati maalumu ili kuhakikisha wanafunzi hawakosi haki yao ya kupata elimu.

Katika maandalizi ya elimu, amesema mkoa unapaswa kuanza mapema kukabiliana na ongezeko la wanafunzi watakaoingia kidato cha kwanza mwaka 2028, kutokana na kuwepo kwa wahitimu wa darasa la sita na la saba.

Amesema mahitaji ya miundombinu yanajumuisha madarasa 1,317, nyumba za walimu na matundu ya vyoo, hivyo viongozi wanapaswa kuweka mipango ya utekelezaji mapema ili kuepusha upungufu wa nafasi za kujifunzia.

Aidha Makalla amewataka viongozi wa wilaya na halmashauri kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unakuwa wa ufanisi, fedha za maendeleo zinafika na kutumika katika miradi iliyokusudiwa, huku usafi wa mazingira na usalama wa wananchi vikipewa kipaumbele.

Amesisitiza kuwa utatuzi wa migogoro na kudumisha amani ni mambo muhimu katika kuweka mazingira rafiki kwa shughuli za kiuchumi na maendeleo ya mkoa.

Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia ni Mbunge wa Arusha Mjini, Paul Christian Makonda, amesema Tanzania inajiandaa kutumia mashindano ya AFCON kama jukwaa la kuitangaza nchi kimataifa, lakini Serikali itahakikisha inafuata masharti ya CAF kabla ya kuanza kutumia nembo na haki za matangazo.

Makonda amesema Tanzania, Kenya na Uganda zimenufaika na mpango wa udhamini unaotoa haki za kutangaza nchi na vivutio vyake kupitia mashindano hayo, huku Serikali ya Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ikiwa imetoa zaidi ya dola milioni 12 kwa ajili ya kupata haki hizo.

Ameeleza kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali tayari imesaini nyaraka zinazohusika kwa upande wake, na kinachosubiriwa ni kukamilika kwa mkataba utakaobainisha masharti ya matumizi ya nembo, rangi na maeneo mengine ya utangazaji yanayoruhusiwa na CAF.

Amesema mara baada ya taratibu hizo kukamilika, Serikali itaanzisha kampeni za kuitangaza Tanzania kupitia mabango, fulana, mabasi yaendayo haraka, treni, televisheni na njia nyingine za mawasiliano, kwa lengo la kuongeza mwonekano wa nchi na kukuza utalii katika soko la kimataifa.

 Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, akizungumza kwenye kikao.hicho jijini Arusha leo