Na Silivia Amandius, Kagera.

Afisa Afya wa Mkoa wa Kagera, Ndugu Yassin Mwinori, amezitaka halmashauri zote nane mkoani humo kuhakikisha shule za bweni zinafanya usafi wa kina na kupulizia dawa za kuangamiza wadudu waharibifu wakiwemo kunguni na viroboto kabla ya Desemba 20 mwaka huu.

Mwinori ameyasema hayo leo Novemba 13, 2026, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, ambapo amesisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kulinda afya za wanafunzi na kuhakikisha wanapata mazingira salama ya kujifunzia na kuishi. Aidha, amewataka wamiliki wa shule kupaka rangi upya mabweni na vitanda pamoja na kuhakikisha usafi unafanyika mara kwa mara.

Ameeleza kuwa agizo hilo linatokana na Sheria ya Afya ya Jamii ya mwaka 2009, kifungu cha 71, kinachowataka wamiliki wa maeneo yenye mikusanyiko ya watu kuhakikisha usafi na udhibiti wa wadudu waharibifu.

Katika hatua nyingine, amewaagiza maafisa afya wa wilaya kukagua maghala ya chakula, kuondoa vyakula vilivyoharibiwa na wadudu, kusafisha vyanzo vya maji na mifereji ya maji ya mvua pamoja na kuhakikisha maji yanayotumiwa na wanafunzi yanatiwa dawa ya klorini.

Amesisitiza kuwa shule zitakazoshindwa kutekeleza agizo hilo hazitaruhusiwa kupokea wanafunzi kuanzia ukaguzi utakaofanyika Desemba 21 hadi Januari 15, mpaka zitakapohakikisha mazingira yake ni salama.

Pia, wamiliki wa shule wanapaswa kuwasilisha vyeti vya uthibitisho wa zoezi la fumigation kutoka kampuni zilizoidhinishwa kisheria.