Ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi, mkoani Mtwara imeweka msukumo katika kushughulikia kero za wananchi wa Tandahimba, baada ya mawaziri kutoa mbele yake ahadi za shilingi bilioni nne kwa mradi wa maji wa Makonde na milioni 600 kwa ujenzi wa kituo cha afya cha Mang’ombya.
Katika mkutano huo, Makamu wa Rais alisisitiza umuhimu wa wananchi kuona matokeo ya utekelezaji wa miradi, akiwapa nafasi mawaziri wenye dhamana kujibu hoja zilizowasilishwa na Mbunge wa Tandahimba, Mhe. Katani Ahmad Katani.
Hatua hiyo iliwezesha wananchi kusikia moja kwa moja majibu ya Serikali kuhusu huduma za afya na maji, pamoja na muda ulioahidiwa wa kufikisha fedha za kuendeleza miradi hiyo.
Kwa upande wa afya, Serikali kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Prof. Riziki Shemdoe, amesema Wizara hiyo itatoa shilingi milioni 600 kwa ujenzi wa kituo cha afya cha Mang’ombya, akieleza kuwa, kwa maelekezo ya Makamu wa Rais, fedha hizo zitafika kabla ya Desemba. Kuhusu kituo cha afya cha Mchichira, Serikali imedhamiria kutafuta fedha za ujenzi wake, na pindi zikipatikana ujenzi utaanza mara moja.
Katika suala la maji, Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amesema Wizara hiyo itatoa kiasi cha bilioni nne ili kumlipa mkandarasi wa mradi wa Makonde kabla ya mwisho wa mwezi novemba ili kuongeza kasi ya utekelezaji. Mradi huo unalenga kuboresha huduma ya maji katika ukanda wa Makonde, ikiwamo Tandahimba na Nanyamba, ambako uchakavu wa miundombinu ya zamani umeelezwa kuwa miongoni mwa changamoto za utoaji wa huduma.
Msisitizo wa Makamu wa Rais katika ziara hiyo ni kutaka kuona matokeo na wananchi wa Tandahimba na Mtwara wanatatuliwa changamoto ya Maji kwa haraka. “Wana Tandahimba hawataki stori. Wana Mtwara hawataki stori. Wanataka kuona matokeo,” alisema.
Akizungumzia majibu yaliyotolewa na mawaziri, Makamu wa Rais alieleza kuwa hoja za mbunge zimepata majibu katika mkutano huohuo na hiyo ndiyo kasi ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Katika kutatua Changamoto za wananchi.
Makamu wa Rais yuko mkoani Mtwara akiendelea na ziara ya kikazi kukagua miradi ya maendeleo na kutatua kero za wananchi.

