Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoani Arusha limeimarisha operesheni ya kuwabaini na kuwachukulia hatua madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka na likizo za wanafunzi.

Akizungumza katika Operesheni hiyo iliyofanyika usiku kuamkia Novemba 13, 2026, Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani mkoani humo, ACP Zauda Mohamed amesema kufuatia ongezeko la abiria na vyombo vya moto barabarani katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka, wameona waimarishe ukaguzi barabarani ili kudhibiti makosa yanayoweza kusababisha ajali.

ACP Zauda amesema katika operesheni wamekagua makosa mbalimbali ikiwemo, mwendo kasi, ulevi, ubovu wa magari, na ukaguzi wa mabasi ya safari ndefu ukifanyika ili kuhakikisha yanakidhi matakwa ya kuwa na madereva wawili kwa ajili ya safari hizo.

Amesema kuwa madereva waliobainika kutokidhi vigezo katika ukaguzi huo, hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwemo kutoa elimu kwa madereva na kuchukua hatua mujibu wa sheria.

Aidha, amewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani na kujiepusha na makosa hatarishi ambayo yamekuwa yakichangia kutokea kwa ajali, akisisitiza umuhimu wa kila mtumiaji wa barabara kuwajibika katika kulinda maisha.

Katika hatua nyingine, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuongeza uangalizi kwa watoto wao katika kipindi hiki cha likizo kinachotarajiwa kudumu takribani miezi miwili, kwa kuhakikisha wanakuwa chini ya uangalizi wanapotumia barabara, iwe kwa kutembea kwa miguu au kusafiri kama abiria.

Kwa wanaomiliki vyombo vya moto, amewataka kuhakikisha wanatunza vizuri funguo za vyombo hivyo sehemu salama zisizofikika kwa watoto, akibainisha kuwa kumekuwa na taarifa za ajali zinazohusisha wanafunzi wanaochukua funguo bila ruhusa na kuendesha vyombo hivyo barabarani.