WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba leo asubuhi (Jumamosi, Novemba 14, 2026) ametembelea kiwanda cha kutengeneza mipira ya kusambazia maji cha MALC kilichopo Kata ya Mlangali, wilayani Ludewa, mkoani Njombe na kukagua uzalishaji kiwandani hapo.

Akizungumza na wafanyakazi wa MALC Investment Company Ltd baada ya kuangalia utendaji kazi wake, Waziri Mkuu amesema amevutiwa na uwekezaji uliofanywa na kazi inayofanyika kwenye kiwanda hicho.

“Nimefurahishwa na kazi inayofanyika kwenye hiki kiwanda. Hongera kwa uthubutu na uwekezaji ulioufanya,” amesema Waziri Mkuu wakati akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Bw. Maiko Lameck Ng’ahala.

Amesema bidhaa wanayozalisha ni ya muhimu kwa sababu inahitajika kwenye miradi ya maji inayojengwa na Serikali. “Kuna miradi iliwahi kukwama kwa sababu ya mabomba kuchelewa kufika kutoka India. Sasa hii ni fursa na ndiyo njia ya kujenga uchumi wa kisasa,” amesema.

Dkt. Mwigulu amesema kuwa nchi nyingi zimeendelea kwa sababu ziliingia kwenye uchumi wa viwanda na na kuamua kufanya uongezaji wa thamani. “Kwetu sisi, njia hii inatusaidia kuongeza ajira na wigo wa kodi na hivyo kuongeza mapato ya nchi,” amesema. 

Mapema, akitoa taarifa kuhusu kiwanda hicho, Bw. Maiko Ng’ahala alisema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho ulianza mwanzoni mwa mwaka 2025 na kilianza rasmi uzalishaji Mei, mwaka huu.

Alisema kiwanda hicho ambacho uwekezaji wake umefikia sh. bilioni 1.2, hivi sasa kinazalisha mipira ya kusambazia maji yenye ukubwa na madaraja mbalimbali ambapo wameanza na daraja “A” na “B” kwa ajili ya kilimo, umwagiliaji na matumizi mengine.

Alisema mbali na kuzalisha mipira ya kusambazia maji yenye ukubwa na madaraja tofauti, lengo kuu la kiwanda hicho ni kuongeza uzalishaji wa bidhaa za ndani, kuchangia maendeleo ya kiuchumi katika Wilaya ya Ludewa na kutoa fursa za ajira ambapo hadi sasa vijana 30 wameajiriwa.