Newala, Mtwara

Makamu wa Rais Mhe. Deogratius Ndejembi,  amepokea kilio cha wananchi wa Newala mkoani Mtwara kuhusu upungufu mkubwa wa maji, ambapo miundombinu iliyopo inazalisha lita milioni 1.5 kwa siku dhidi ya mahitaji ya zaidi ya lita milioni sita.

Akizungumza katika mkutano na wananchi, Makamu wa Rais amesikiliza changamoto hiyo iliyowasilishwa na Mbunge wa Newala Mjini, Rashid Mohamed Mtima, na Mbunge wa Newala Vijijini, Dkt. Yahya Esmail Nawanda.

Wabunge hao wameeleza kuwa wananchi bado wanategemea mradi uliojengwa mwaka 1954,wakati wa utawala wa Awamu ya kwanza, ambao uwezo wake haukidhi mahitaji ya sasa, na kuiomba Serikali kuharakisha hatua za kuondoa adha hiyo.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri wa Maji kueleza namna walivyojipanga kutatua changamoto hiyo,  Makamu wa Rais ameeleza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kutatua kero za wananchi na hasa dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.  

iAkitoa majibu mbele ya Makamu wa Rais, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa maji wa Mitema kwa fedha kwa ndani, huku ujenzi wa visima na matanki ukiendelea.

Amesema mkandarasi wa mradi huo anadai Shilingi bilioni nane, na kuahidi kuhakikisha malipo hayo yanalipwa kwa Awamu mbili  ili kazi ziendelee na mradi ukamilike kwa wakati.

Kuhusu kilimo cha korosho, Makamu wa Rais amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia upatikanaji wa salfa yenye ubora ili kuongeza uzalishaji na kuwawezesha wakulima kunufaika na zao hilo.

Ameonya kuwa Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayebainika kuchakachua pembejeo au kutumia ruzuku kujinufaisha kwa kuwaumiza wakulima, huku akisisitiza uchunguzi wa malalamiko kuhusu pembejeo kutotoa matokeo yaliyotarajiwa.

Amesema ruzuku inayotolewa na Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga kuinua kipato cha wakulima, hivyo ni lazima pembejeo ziwafikie kwa wakati na zikiwa na ubora unaotakiwa.

Katika suala la ardhi, Makamu wa Rais amegusia migogoro kati ya wakulima na wafugaji, akisisitiza umuhimu wa kuipatia ufumbuzi ili wananchi waendelee na shughuli zao kwa amani.

Aidha, amezungumzia kukamilika kwa barabara ya Masasi -Newala – Mtwara kama sehemu ya hatua zilizopigwa katika kuboresha miundombinu ya usafiri mkoani humo.