Wakili Mkuu wa Serikali, Ally Possi akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha 

………

Na Happy Lazaro, Arusha

Wakili Mkuu wa Serikali, Ally Possi, amesema uhaba wa fedha unaoikabili Jumuiya ya Afrika Mashariki umekuwa kikwazo katika utekelezaji wa majukumu yake, hali iliyosababisha kudorora kwa shughuli muhimu za taasisi mbalimbali zilizo chini ya jumuiya hiyo, ikiwemo Bunge na Mahakama ya Afrika Mashariki.

Possi amesema kutokana na changamoto hiyo, baadhi ya shughuli za jumuiya zimeshindwa kufanyika kama ilivyopangwa, huku vikao vya Bunge la Afrika Mashariki na Mahakama vikikosekana kutokana na kukosekana kwa rasilimali fedha za kutosha kuendesha shughuli hizo.

Ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akizungumza katika maadhimisho ya miaka 25 ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki yaliyofanyika katika makao makuu ya jumuiya ya Afrika Mashariki.

Amesema kuwa, hali hiyo pia imeathiri utendaji wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo idadi ya wafanyakazi imepungua kwa kiwango kinachofanya baadhi ya majukumu ya taasisi hiyo kushindwa kutekelezwa ipasavyo.

Ameongeza kuwa, upungufu huo wa watumishi unaathiri uwezo wa Sekretarieti kuratibu na kusimamia shughuli za kila siku za jumuiya, jambo linaloweza kudhoofisha utekelezaji wa malengo yaliyowekwa na nchi wanachama kupitia ushirikiano wa kikanda.

Akifafanua ukubwa wa changamoto hiyo, Possi amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki imekuwa bila Mwanasheria Mkuu tangu Mei mwaka 2025, baada ya aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo kumaliza muda wake wa utumishi, lakini hadi sasa nafasi hiyo haijajazwa.

Amesema kukosekana kwa Mwanasheria Mkuu wa Jumuiya kwa kipindi hicho ni moja ya changamoto zinazoonyesha namna uhaba wa rasilimali unavyoweza kuathiri utendaji wa taasisi za kikanda zinazopaswa kusimamia masuala ya kisheria na utekelezaji wa Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Possi amesema kuwa, umuhimu wa nchi wanachama kuhakikisha zinatimiza wajibu wao wa kuchangia fedha za kuendesha jumuiya ili taasisi zake ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Amesisitiza kuwa upatikanaji wa fedha za kutosha ni muhimu katika kuimarisha taasisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, ikiwemo Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki, ili ziweze kutekeleza majukumu yake ya kisheria, kusimamia haki na kuendeleza mtangamano wa kikanda kwa manufaa ya nchi wanachama na wananchi wake.