📌Akutana menejimenti na wafanyakazi wa BRELA na Kawaasa kufanya kazi kwa weledi; 

📌 Awataka kuhakikisha Leseni za biashara kundi A hazitolewi kiholela, hasa kwa wafanyabiashara kutoka nje ya nchi na kwa wale waliopewa leseni awali kutohuisha leseni Hizo mara zitakapoisha muda wake;

📌 Ahimiza nidhamu ndani ya taasisi na watumishi kufuata taratibu za kazi.

📌 Atoa rai kwa wasanii kusajili bunifu zao ili kulindwa kisheria  

 DAR ES SALAAM

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe Balozi Waziri Rajab Salum ameielekeza BRELA kutohuisha Leseni za Biashara Kundi A kwa wageni kwa aina za biashara zilizokatazwa ili kulinda biashara za wazawa na kwa waliopewa Leseni awali kabla ya katazo pindi Leseni hizo zitakapo kwisha muda wake kutozihuisha tena. Mhe Balozi Waziri ameyasema hayo leo alipofanya ziara katika ofisi za BRELA na kufanya mazungumzo na menejimenti pamoja na wafanyakazi ambapo amesisitiza kuwa katazo hilo limetolewa na Serikali ili kuwalinda wafanyabiashara wa Kitanzania na haitabadili maamuzi hayo  

Aidha Balozi Waziri akiwa BRELA alipata nafasi ya kujionea namna watumishi wanavyochakata maombi kutoka Kurugenzi ya kampuni na Majina ya Biashara, namna mifumo inavyolindwa na utunzaji wa majalada ya taarifa za wafanyabiashara  

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Katibu Mkuu amehimiza kuimarishwa kwa ushirikiano baina ya Bodi, Wizara, Menejimenti na wadau wengine, huku akisisitiza umuhimu wa watumishi kuaminiana, kupendana na kuzingatia nidhamu katika utekelezaji wa majukumu yao. 

Aidha asisitiza vijana wabunifu na wasanii kulinda bunifu zao kisheria ili haki zao zisipotee maana bunifu hizo ndio chanzo cha biashara na kuwainua katika vipato vyao huku Wizara ya Viwanda na Biashara ikiendelea na maandalizi ya kuwa na sera ya biashara bunifu  

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, amesema taasisi hiyo inasimamia sheria sita zinazohusu usajili wa majina ya biashara na kampuni, haki miliki bunifu, hataza, leseni za biashara na leseni za viwanda.  

Ameeleza kuwa BRELA inaendelea kuboresha mifumo ya TEHAMA na kutoa elimu kwa wadau kuhusu taratibu za usajili na huduma zinazotolewa na taasisi hiyo. 

Ziara hiyo imelenga kuimarisha usimamizi wa Wizara katika taasisi zilizo chini yake, kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu na utoaji wa huduma kwa wananchi.