Na Mwandishi Maalumu,  Dar es Salaam

Wafanyakazi wa NMB Bank wametakiwa kujenga utamaduni wa kuchunguza afya zao angalau mara moja kwa mwaka ili kubaini mapema viashiria vya magonjwa ya saratani na kuchukua hatua stahiki za matibabu.

Wito huo umetolewa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Afisa wa rasilimali watu wa NMB Bank Makau Makuu Pascal Itangaja, wakati wa kilele cha maadhimisho ya mwezi wa uhamasishaji na utoaji elimu kwa magonjwa ya saratani kwa wafanyakazi wa Bank hiyo.

Maadhimisho hayo yalienda sambamba na utoaji wa huduma za uchunguzi wa awali wa saratani za matiti, mlango wa kizazi na tezi dume kwa wafanyakazi wa benki hiyo.

Itangaja alisema wataalamu kutoa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) wamefanya kambi maalum ya siku tatu ya kuhakikisha wafanyakazi wa benki hiyo wanafanya uchunguzi wa saratani.

“Kufanyika kwa kambi hiyo kulikuwa ni muhimu kwa sababu kumewawezesha wafanyakazi kufahamu hali zao za afya na kuchukua hatua zinazostahili kwa wakati, bila kulazimika kuacha majukumu yao ya kikazi ili kufuata huduma hizo katika vituo vya afya.”

“Kufahamu hali ya afya mapema kunarahisisha upatikanaji wa matibabu kwa wakati na kuwawezesha wafanyakazi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.”

Itangaja alisema, “NMB Bank itaendelea kushirikiana na Taasisi ya saratani Ocean Road (ORCI) katika kuandaa programu nyingine za uchunguzi wa afya ikiwemo uchunguzi wa homa ya ini, pamoja na kutoa chanjo kwa wale ambao watakutwa hawana tatizo.”

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Nelson Eliaman alisema lengo la zoezi hilo ni kufanya uchunguzi wa awali ili kubaini viashiria vya uwepo wa saratani, na kutoa rufaa kwa ajili ya uchunguzi zaidi kwa wale wataokutwa na changamoto.

Dkt. Eliaman alieleza kuwa saratani za matiti, mlango wa kizazi na tezi dume zimepewa kipaumbele katika zoezi hilo kutokana na kuwa miongoni mwa saratani  zinazochangia idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.

Alisema Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) imeamua kufikisha huduma hizo katika ofisi za NMB Bank Makao Makuu kwa kuzingatia majukumu ya kikazi ya wafanyakazi hao, ambayo wakati mwingine yanaweza kuwafanya washindwe kupata nafasi ya kufika katika Taasisi hiyo kwa ajili ya uchunguzi.

“Ninawahimiza wananchi na wafanyakazi wa taasisi mbalimbali kuweka utaratibu wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara, ikiwemo ugonjwa wa saratani kwani  saratani inatibika kama magonjwa mengine”, aisema Dkt. Eliaman.

Nao wafanyakazi wa NMB waliopata huduma za uchunguzi wa afya walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia kufahamu hali za afya zao.

“Nilikuwa na hofu ya kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya matiti na mlango wa kizazi nikidhani vipimo hivyo vina maumivu na kuchukua muda mrefu, Baada ya kupata huduma  nimebaini vipimo hivyo ni vya kawaida ninawasihi wanawake wenzangu kufanya uchunguzi bila ya kuwa na hofu”, alisema mfanyakazi wa benki hiyo.

“Nimefurahishwa na huduma ya uchunguzi wa saratani ya tezi dume inayotumia teknolojia ya kisasa, ambapo damu huchukuliwa kwa kuchomwa kwenye kidole na majibu kupatikana ndani ya dakika tano jambo lililonisaidia kuondoa hofu niliyokuwa nayo awali kuhusu vipimo hivi,” alisema Salum Seif kutoka Idara ya Product and Digital Bank.