Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Nov 11,2026
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini, Silvestry Koka, amechangia sh 500,000 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni katika Shule ya Sekondari Mwambisi iliyopo Kata ya Kongowe, Wilaya ya Kibaha.
Koka ametoa mchango huo wakati wa mahafali ya 11 ya shule hiyo, akisema wadau wa elimu wanapaswa kushirikiana kuchangia maendeleo ya sekta hiyo ili kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira bora.
Amesema mchango wake unalenga kuwa chachu ya kufanikisha ujenzi wa mabweni hayo na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Mkuu wa Shule hiyo, Philemon Fredy, amemshukuru mbunge huyo kwa mchango huo, akieleza kuwa utasaidia kuanza kwa mradi wa ujenzi wa mabweni huku baadhi ya vifaa vya ujenzi vikiwa tayari vimepatikana.
Mpango wa shule hiyo ni kujenga mabweni manne ili kuboresha mazingira ya wanafunzi ambapo michango iliyopatikana ni pamoja na matofali 2,500 na mifuko 33 ya saruji, huku thamani ya michango yote iliyotolewa ikifikia Sh milioni tatu.

