……….

Na  Mwamvua Mwimgi Pwani 

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, ameitaka RUWASA kuimarisha uendeshaji wa huduma ya maji kwa kuzingatia misingi ya kibiashara, ikiwemo kuongeza mapato kupitia kuwafikishia huduma wawekezaji wanaohitaji maji kwa shughuli za uzalishaji.

Amesema Mkoa wa Pwani unaendelea kukua katika uwekezaji wa viwanda, hali inayoongeza mahitaji ya maji na kuifanya RUWASA kuwa na umuhimu wa kuweka mikakati ya kuhakikisha maeneo ya uwekezaji yanapata huduma ya uhakika huku taasisi hiyo ikiongeza mapato yake.

Nyongo ametoa maelekezo hayo Novemba 11, 2026, katika mkutano kati ya RUWASA na uongozi wa Mkoa wa Pwani uliofanyika katika ukumbi mdogo wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, akieleza kuwa wawekezaji ni wateja wazuri ambao wanaweza kuchangia mapato kupitia huduma ya maji kwa matumizi ya kibiashara.

Amesema wakati Serikali ikiendelea kuwekeza fedha katika miradi ya maji, bado mahitaji ya huduma hiyo ni makubwa, hivyo RUWASA inapaswa kuimarisha mikakati ya kuwahudumia wananchi na wawekezaji ili wote wanufaike na rasilimali hiyo kwa shughuli zao za kila siku na uzalishaji.

Aidha, ameitaka RUWASA Wilaya ya Mkuranga kutafuta suluhu ya changamoto za upatikanaji wa maji katika maeneo yake, akisisitiza wananchi wapate maji safi na salama badala ya kutegemea vyanzo visivyo salama.

Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Pwani, Upendo Lugongo, amesema upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa vijijini umefikia asilimia 84.3, huku wakala huo ukiendelea kutekeleza Programu ya 1575 inayolenga kufikisha huduma ya maji katika vijiji 13 katika mwaka wa fedha 2026/2027, kati ya vijiji 22 vilivyo kwenye programu hiyo.

Amesema vijiji hivyo vipo katika Halmashauri za Rufiji (1), Kibiti (3), Kisarawe (3), Mkuranga (3) na Mafia (3), huku RUWASA ikiendelea kutekeleza miradi 36 ya maji katika hatua mbalimbali na kuandaa utekelezaji wa miradi mipya 24.

Katika mwaka wa fedha 2026/2027, RUWASA Mkoa wa Pwani imetengewa shilingi bilioni 14.64, ambapo shilingi bilioni 5.51 zitatumika kutekeleza miradi 36 inayoendelea na shilingi bilioni 9.13 kuelekezwa kwenye miradi mipya 24. Miradi 36 ikikamilika inatarajiwa kuwafikishia huduma ya maji wananchi 141,950, sawa na asilimia 5.5 ya wakazi wa mkoa huo.