Rais wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) Jaji Nestory Kayobera, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo .
………
Na Happy Lazaro, Arusha
Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda, Rebecca Kadaga, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 25 ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ), yatakayofanyika Novemba 12, mwaka huu, katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha.
Rais wa Mahakama hiyo, Jaji Nestory Kayobera, amesema maadhimisho hayo yanalenga kutathmini mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 25, hali ya sasa ya Mahakama hiyo pamoja na mipango ya baadaye katika kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Amesema maadhimisho hayo yatafanyika chini ya kauli mbiu isemayo “Kutoka Misingi Hadi Mustakabali”, huku yakiambatana na mijadala mbalimbali itakayojikita katika mchango wa Mahakama katika maendeleo ya Jumuiya, usuluhishi wa migogoro ya kibiashara na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.
Jaji Kayobera amesema Mahakama hiyo imeendelea kuwa nguzo muhimu katika utoaji wa haki kwa wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kutoa fursa kwa watu binafsi, mashirika ya kiraia, vyama vya siasa, vyombo vya habari na serikali kuwasilisha mashauri yao.
Amesema hatua zilizofikiwa katika kipindi hicho zinaonesha mchango wa Mahakama katika kuhakikisha haki inatendeka na taasisi hiyo inaendelea kuimarika katika kutekeleza majukumu yake.
Aidha, amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye nchi wanachama nane na idadi ya watu inayozidi milioni 350 imeendelea kunufaika na uwepo wa Mahakama hiyo kupitia utatuzi wa mashauri mbalimbali yanayowasilishwa mbele yake.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 25, Mahakama hiyo imeendelea kutekeleza wajibu wake wa kutatua migogoro na kuimarisha misingi ya haki, hatua inayochangia kuendeleza ushirikiano na maendeleo ya kikanda.
Maadhimisho hayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na wageni zaidi ya 200 kutoka ndani na nje ya nchi wanachama, wakiwemo majaji wakuu, mawaziri wa Sheria, wanasheria wakuu wa serikali pamoja na wasomi kutoka Afrika na Marekani.
