Meneja Mwandamizi wa Biashara kutoka PASS Trust, Mbwaike Mahyenga akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha.
Meneja wa kitengo cha Masoko, Biashara na Uwekezaji TAHA,Dkt .Steven Tumaini , akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho hayo jijini Arusha .
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha .Taasisi ya PASS TRUST kwa kushirikiana na TAHA zimeweka mikakati ya kuunganisha wakulima, wafanyabiashara, taasisi za kifedha na wawekezaji ili kuongeza mitaji na kukuza sekta ya mazao ya bustani nchini.
Akizungumza katika maonesho ya HortiLogistics Africa 2026 yanayofanyika jijini Arusha, Meneja Mwandamizi wa Biashara kutoka PASS Trust, Mbwaike Mahyenga amesema lengo ni kuwakutanisha wadau wote wa mnyororo wa thamani ili kujadili namna bora ya kuongeza uwekezaji katika sekta hiyo.
Amesema katika mkutano huo wamewashirikisha mabenki, wadau wa masoko na watunga sera wakiwemo kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania ili kujadili namna ya kushirikiana kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wakulima na wafanyabiashara.
Ameongeza kuwa upatikanaji wa mitaji ni muhimu katika kuongeza uzalishaji, kuboresha biashara na kuwezesha wadau wa hortikacha kufanya kazi kwa pamoja ili kufikia malengo ya maendeleo yaliyowekwa na Serikali kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Meneja wa kitengo cha Masoko, Biashara na Uwekezaji TAHA,Dkt .Steven Tumaini , amesema uwekezaji wa PASS katika sekta hiyo utasaidia kuboresha usafirishaji, uhifadhi wa mazao na kuongeza tija kwa wakulima.
Amesema PASS inaunga mkono upatikanaji wa magari maalumu yenye mifumo ya kuhifadhi ubaridi (Perishable Trucks), yatakayosaidia kupunguza uharibifu wa mazao kuanzia shambani hadi sokoni.
Ameongeza kuwa uwekezaji katika miundombinu ya kuhifadhi na kukusanya mazao (Pack Houses na Aggregation Centres), matrekta pamoja na mifumo ya umwagiliaji wa matone utasaidia kuongeza uzalishaji na kupunguza upotevu wa maji.
Amefafanua kuwa,PASS inawawezesha pia wafanyabiashara wa pembejeo na viuatilifu pamoja na wahandisi wanaotoa huduma za kitaalamu, huku ikiunga mkono maonesho yanayounganisha wadau wa mnyororo mzima wa thamani.
“TAHA, ambayo imefikisha miaka 20 ya kuendeleza sekta ya hortikacha, itaongeza mafunzo na usambazaji wa taarifa kwa wakulima kuhusu mahitaji halisi ya wanunuzi ili wazalishe mazao yanayokidhi viwango vya masoko.”amesema Dkt.Tumaini .
Amefafanua kuwa ,TAHA pia inaanzisha mfumo wa Perishable Observatory System utakaowaunganisha wadau na kurahisisha upatikanaji wa taarifa kuhusu mahitaji ya masoko, changamoto na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kukuza sekta hiyo nchini.
