Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo ,Emmanuel Mamuya, akizungumza na waandishi ww habari katika maonesho ya Jukwaa la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji wa Mazao ya Bustani, HortiLogistica Africa yanayoendelea jijini Arusha

…………

Na Happy Lazaro, Arusha 

Kampuni ya Milele Oils Ltd imewahimiza wakulima wa zao la parachichi katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kuongeza uzalishaji wa zao hilo, ikieleza kuwa uwepo wa kiwanda cha kuchakata parachichi na kuzalisha mafuta jijini Arusha ni fursa muhimu ya kukuza uchumi wa wakulima.

Kampuni hiyo inayojishughulisha na uzalishaji wa mafuta ya parachichi imeanzisha kiwanda chake eneo la Njiro jijini Arusha, ikiwa na lengo la kuongeza thamani ya zao hilo na kuwaunganisha wakulima na soko la uhakika.

Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo ,Emmanuel Mamuya, wakati akizungumza katika maonesho ya Jukwaa la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji wa Mazao ya Bustani, HortiLogistica Africa 2026,linalofanyika katika viwanja vya TGT jijini Arusha.

Mamuya amesema uamuzi wa kuanzisha kiwanda Arusha umetokana na umuhimu wa mji huo katika shughuli za biashara na usafirishaji, pamoja na kuwa karibu na maeneo yanayozalisha parachichi.

Mamuya amesema kampuni hiyo inanunua parachichi kutoka kwa wakulima wakubwa, vyama vya ushirika vya akiba na mikopo (SACCOS), pamoja na mtandao wa madalali, ambapo hununua kwa kuzingatia bei iliyopo sokoni.

Amesema baada ya kununuliwa, parachichi hupelekwa kiwandani kwa ajili ya maandalizi na hatua mbalimbali za uchakataji, ikiwemo kuyaacha yaive, kuyasaga na hatimaye kuyakamua ili kupata mafuta yanayozalishwa kwa wingi.

“Mafuta yanayozalishwa na kampuni hiyo huuzwa kwa jumla na kusafirishwa kwenda katika masoko ya nje ya nchi, akieleza kuwa mahitaji ya bidhaa hiyo katika soko la kimataifa yanaendelea kutoa fursa kwa wakulima na wawekezaji.”amesema Mamuya.

Akizungumzia mwenendo wa soko, Mamuya amesema katika kipindi cha miezi miwili iliyopita soko la parachichi lilishuka, lakini kwa sasa bei zimeanza kuimarika na anatarajia shughuli za soko kuongezeka zaidi mwezi Desemba.

Amesema kutokana na mahitaji makubwa ya parachichi na bidhaa zake katika masoko ya nje, wakulima hawapaswi kukata tamaa kutokana na mabadiliko ya bei ya muda mfupi, bali waendelee kuongeza uzalishaji ili kunufaika na fursa zilizopo, akisisitiza kuwa soko lipo na wanapaswa kuendelea kufanya kazi kwa bidii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha wa kampuni hiyo, Crispin Nkya amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuchakata hadi tani sita za parachichi kwa saa, hatua inayotoa nafasi kwa wakulima wengi kuuza mazao yao bila kulazimika kuyasafirisha umbali mrefu.

Nkya amesema wakulima wa Arusha na Kilimanjaro wanapaswa kutumia fursa hiyo kwa kupeleka parachichi zao kiwandani, bila kujali ukubwa wa mashamba yao, kwani kampuni ipo tayari kushirikiana na wakulima wadogo na wakubwa.

Amesema hapo awali baadhi ya wakulima walilazimika kusafirisha parachichi kwenda Njombe au hata Nairobi nchini Kenya kutafuta huduma za masoko na uchakataji, lakini uwepo wa kiwanda hicho Arusha unapunguza changamoto ya umbali na gharama za usafirishaji.

Amesisitiza kuwa wakulima wanapaswa kulitazama zao la parachichi kama fursa ya kiuchumi, kwani uchakataji wake kuwa mafuta unaongeza thamani ya mazao na kufungua njia nyingine za kibiashara badala ya kutegemea soko la matunda ghafi pekee.