NA DENIS MLOWE, IRINGA

WATU 21 wamefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa katika ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha basi la abiria la Kampuni ya Maokoto Bus Services na lori la mizigo katika eneo la Njiapanda ya Kiponzero, Masumbo, kwenye barabara kuu ya Iringa–Mbeya.

Ajali hiyo imetokea majira ya saa moja asubuhi, wakati basi hilo lililokuwa likitoka Kijiji cha Wasa, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, kuelekea Iringa Mjini lilipogongana na lori lililokuwa likipita katika barabara hiyo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi alisema watu 21 waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni wanaume 10, wanawake tisa na watoto wawili, huku majeruhi watano wakikimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.

Alisema kuwa taarifa za awali za uchunguzi zinaeleza kuwa ajali hiyo huenda ilisababishwa na hitilafu katika mfumo wa breki za basi, hali iliyomfanya dereva kushindwa kulidhibiti kabla ya kugongana na lori hilo.

Hata hivyo, taarifa za Polisi zimeeleza kuwa mazingira ya ajali hiyo yanaendelea kufanyiwa uchunguzi ili kubaini chanzo chake kwa uhakika.

Katika hatua nyingine, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameeleza kupokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vifo vya watu hao na kutuma salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, pamoja na familia, ndugu na jamaa wa wote waliopoteza maisha.

Katika salamu zake, Rais Samia amesema:

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya ndugu zetu 21 vilivyotokana na ajali ya barabarani iliyohusisha basi la abiria na lori la mizigo katika eneo la Masumbo, Barabara ya Iringa–Mbeya, mkoani Iringa, leo.”

Ameendelea kutoa pole kwa wafiwa na kuwaombea faraja, subira na nguvu katika kipindi hiki kigumu, huku akiwaombea majeruhi wote wapone haraka.

Aidha, Rais Samia ameomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi.

Kwa upande wa majeruhi, taarifa zilizotolewa zimeeleza kuwa wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Hospitali Teule ya Ipamba na Zahanati ya Masumbo iliyopo Ifunda, huku miili ya marehemu ikihifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.

Wakati huo huo, tukio hilo limeibua majonzi kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa na maeneo mengine kutokana na idadi kubwa ya watu waliopoteza maisha, wakiwemo watoto wawili.

Jeshi la Polisi limeendelea kutoa wito kwa madereva kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, kuhakikisha vyombo vya moto vinakuwa katika hali nzuri na kuchukua tahadhari wanapotumia barabara ili kuepusha ajali zinazoweza kusababisha vifo na majeraha.

Marehemu wote wanakumbukwa katika kipindi hiki cha majonzi, huku familia zilizopoteza wapendwa wao zikiendelea kuhitaji faraja na msaada.