Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na mlezi wa kampeni ya Afya Bora, Maisha Bora, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, akimkabidhi Afisa Mtendaji Mkuu wa Yas Tanzania, Bw. Pierre Canton Bacara, tuzo ya kutambua mchango wa Yas, wakati wa hafla ya kufunga kambi ya sita ya matibabu ya kampeni hiyo iliyofanyika Novemba 7 katika viwanja vya Kinduni Academy, Mkoa wa Kaskazini Unguja. Wanaoshuhudia ni Waziri wa Afya Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui (wa pili kutoka kushoto), Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Dkt. Riziki Pembe Juma (kushoto), na Afisa Mtendaji Mkuu wa Zanzibar Maisha Bora Foundation, Bi. Rehema Tukai (kulia). Katika hafla hiyo iliyohitimisha kambi ya siku tano, Yas iliahidi kuendelea kuunga mkono kampeni hiyo kwa miaka mitatu ijayo.

Kinduni, Zanzibar, Novemba 7, 2026. Kampuni ya mawasiliano ya Yas Tanzania imeahidi kuendelea kuunga mkono kampeni ya Afya Bora, Maisha Bora iliyo chini ya taaisisi ya Zanzibar Maisha Boara Foundation kwa miaka mitatu ijayo ili wananchi wengi zaidi Zanzibar waweze kunufaika na huduma za uchunguzi na matibabu bila malipo.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Yas Tanzania, Bw. Pierre Canton Bacara, ametangaza ahadi hiyo siku ya leo 07.11.2026, wakati wa kufunga kambi ya sita ya matibabu ya kampeni hiyo katika viwanja vya Kinduni Academy, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Akifunga kambi hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, ambaye pia ni mlezi wa kampeni hiyo, alisema kwa siku tano wakazi wa eneo hilo wamepata fursa ya kuonana na madaktari, kufanyiwa uchunguzi na kupata matibabu bila malipo.

Mhe. Abdulla alimpongeza Mwenyekiti wa ZMBF, Mama Mariam Mwinyi, kwa kufikisha huduma hizo katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar. Pia aliishukuru Yas kwa kudhamini kambi ya Kinduni na ahadi yao ya kuunga mkono kampeni hiyo kwa miaka mitatu ijayo. Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na kuziunga mkono taasisi ambazo zinazoleta huduma za kijamii karibu zaidi na wananchi.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, alisema zaidi ya watu 4,200 walifika kambini katika siku nne za kwanza. Amewahimiza wale waliobainika kuwa na tatizo la kiafya wakati wa uchunguzi kufika mapema katika kituo cha afya au hospitali ili waendelee kupata huduma kabla hali zao hazijawa mbaya.

Akiwasilisha taarifa ya kitaalamu ya kambi hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Mngereza Mzee Miraji, alisema serikali inalenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030, aina zote za huduma za uchunguzi wa magonjwa na matibabu ya kibingwa zinapatikana Zanzibar. Alisema hatua hiyo itapunguza gharama wanazobeba wagonjwa wanaolazimika kusafiri nje ya Zanzibar kufuata matibabu.

Mapema mwezi Mei mwaka huu, Dkt. Miraji alitangaza kuwa serikali inapanga kutumia shilingi trilioni moja kwa ajili ya huduma za afya kuanzia mwaka 2026 hadi 2030. Sehemu ya fedha hizo itatumika kuboresha vituo vya kutolea huduma za afya na kuimarisha huduma za afya ya msingi

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Yas Bw. Pierre Canton Bacara alimshukuru Mama Mariam Mwinyi kwa kuikaribisha Yas kuwa mshirika rasmi wa kambi hiyo na kuongeza kuwa “Kwa miaka mitatu ijayo, tutaendelea kushirikiana na Zanzibar Maisha Bora Foundation ili kambi hii ifanyike kila mwaka na kuwafikia Wazanzibari wengi zaidi,” alisema.

Yas pia ilitoa kiti cha matibabu ya meno pamoja na vifaa vyake na vishikwambi (tablets) 30 kwa matumizi ya wahudumu wa afya baada ya kambi kumalizika. Bw. Bacara aliongeza kuwa kupitia kampeni ya Tumaini, wafanyakazi wa Yas wameweza kusaidia kuboresha huduma za afya ya uzazi katika hospitali ya Mwera Pongwe, Unguja, na Hospitali ya wilaya ya Kinyasini, Pemba. Alisema zaidi ya akina mama 3,000 wamenufaika na kampeni hiyo kwa Zanzibar pekee.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa ZMBF, Bi. Rehema Tukai, alisema ushirikiano na Wizara ya Afya uliwawezesha wataalamu katika kambi ya Kinduni kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo na saratani, kufanya upasuaji mdogo na kutoa huduma za afya ya uzazi, macho na ngozi. Alisema taasisi hiyo itaendelea kuandaa kambi katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Hafla ya kufunga kambi hiyo pia iliambatana na uzinduzi wa Build Resilience, kampeni ya Umoja wa Wake wa Marais wa Afrika kwa Maendeleo (OAFLAD).