Baadhi ya wakazi wa Mbinga wakisubiri Matibabu katika Hospitali ya wilaya Mbuyula
Na Mwandishi wetu, Mbinga
BAADHI ya wakazi wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma,wameipongeza Serikali kupitia Halmashauri ya mji Mbinga kwa uboreshaji wa huduma ya afya ikiwemo vifaa tiba na ujenzi wa majengo ya kisasa ya kutolea huduma hizo katika Hospitali ya wilaya Mbuyula.
Wamesema,uboreshaji uliofanyika umemaliza changamoto kubwa ya kutembea umbali mrefu hadi Hospitali ya misheni Litembo,St Joseph Peramiho na Hospitali teule ya rufaa ya Mkoa iliyopo Songea mjini umbali wa kilometa 100 ili kupata huduma,ambazo sasa zinapatikana katika Hospitali hiyo.
Mkazi wa mtaa wa Kipika Ernest Kapinga,amefurahishwa na maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali hususani ujenzi wa majengo mapya ya kutolea huduma za afya ikiwemo jengo la wagonjwa wa nje(OPD),maabara ambapo awali kulikuwa na majengo yaliyochakaa kutokana na kujengwa muda mrefu.
Alisema,huduma zinatolewa katika Hospitali hiyo ni nzuri na kuipongeza Serikali kwa jitihada zake za kuboresha miundombinu pamoja na kuleta vifaa tiba vikiwemo vipimo vya uchunguzi na vifaa vingine vya kutolea huduma za matibabu.
“Tunamshukuru sana Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kutujali sisi wananchi wanyonge,tunafurahishwa na mazingira safi na huduma bora zinazotolewa katika Hospitali hii,sasa mazingira yameboreshwa ikilinganishwa na hapo awali,miaka ya nyuma kulikuwa na vipimo vidogo vidogo na vikubwa tulikuwa tunapata kutoka nje ya Mbinga”alisema Kapinga.
Mkazi wa Litembo Elenzian Kapinga,ameiomba Serikali kuongeza watumishi ambao watasaidiana na waliopo ili kutoa huduma bora zaidi na haraka kwa wagonjwa wanaofika kupata matibabu katika Hospitali hiyo ambayo ni mkombozi kwa maisha ya wananchi wa Mbinga na wilayani jirani ya Songea na Nyasa.
“Tunaipongeza sana Serikali yetu ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa maboresho katika Hospitali yetu ya wilaya,lakini tunaomba tuongezewe watumishi ambao wataongeza nguvu kutoa huduma kwa haraka ili kupunguza muda wa kusubiri huduma”alisema Kapinga.
John Kiwili,amepongeza utaratibu mzuri kwa wagonjwa ikiwemo utengwa dirisha maalum kwa ajili ya wazee,hata hivyo ameshauri kuletwa madaktari bingwa wa magonjwa ya macho na masikio ili waweze kuwasaidia wananchi wenye changamoto hizo.
Kwa upande wake msimamizi wa huduma za maabara katika ya Mbuyula James Samweli,ameishukuru serikali kwa hatua inazochukua kuboresha miundombinu ikiwemo jengo jipya la huduma za maabara ambalo limewapa morali ya kufanya kazi na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Alisema,maboresho yaliyofanyika katika Hospitali hiyo yataondoa msongamano wa wagonjwa ikilinganisha na jengo ya zamani ambalo halikuwa na sifa na vigezo vya kuwa maabara,hivyo ilikuwa changamoto kufanya kazi kwa ufanisi.
“Tangu jengo hili lilipoanza kutumika huduma nyingi zimeboreshwa kwani awali ilikuwa rahisi sampuli kupoteza kutokana na namna ujenzi ulivyokuwa,lakini kutokana na maboresho haya sio rahisi kupoteza sampuli”alisema.
Alieleza kuwa,sasa wanaotesha wadudu wanaotambua aina ya vimelea vya ugonjwa kutokana na uwepo wa mashine za kisasa zenye uwezo mkubwa,kufanya vipimo vya kupandisha homoni za uzazi kwa wanawake,na watumishi wanafanya kazi kwa ufanisi,uhuru na kutoa majibu ya uhakika kwa wagonjwa.
Mratibu wa huduma za bima ya afya katika Hospitali ya Mbuyula Richard Msimbila,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha huduma za afya katika Hospitali hiyo kwani ukarabati uliofanyika umewezesha kutimiza malengo waliyojiwekeaya utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Alisema,majengo mapya yamesaidia hata kurudisha wateja(wagonjwa)waliokwenda hospitali nyingine,hata hivyo wameanza kurudi kupata huduma Hospitali ya Mbuyula baada ya maboresho hayo makubwa.
Miongoni mwa majengo mapya ya kutolea Huduma za matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mbinga maarufu Mbuyula
