Mkurugenzi wa Shule ya Joan Vision Grace Quintine akizungumza kwenye Mahafali ya nne ya Shule hiyo,kushoto Afisa Maendeleo ya jamii Halmashauri ya Mji Mbinga Secy Mbata
Na Mwandishi wetu,Mbinga
MKURUGENZI wa Shule ya Joan Vision, Grace Quintine amewashukuru wazazi na walezi kwa kuendelea kuiamini shule hiyo, huku akiwataka kuendeleza ushirikiano na shule katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora na matokeo mazuri zaidi.
Akizungumza katika mahafali ya nne ya shule hiyo, Grace amesema mafanikio na matokeo mazuri yaliyopatikana ni matokeo ya ushirikiano kati ya walimu, wazazi na wanafunzi, hivyo amewahimiza wazazi kuendelea kuwa na imani na shule hiyo
Aidha, amewataka wazazi na walezi kuendelea kuwasimamia watoto wao wanapokuwa nyumbani wakati wa likizo kwa kuhakikisha wanaendelea kujisomea ili wasipoteze mwelekeo wa masomo.
Amesisitiza kuwa uongozi wa shule hiyo uko tayari kushirikiana bega kwa bega na wazazi katika kuhakikisha watoto wanapata ufaulu bora zaidi.
Shule ya Joan Vision inapatikana Kata ya Masumuni, Mtaa wa Mji Mwema, ikiwa na mazingira mazuri ya kujifunzia pamoja na ulinzi wa kutosha kwa ajili ya kuhakikisha watoto wanapata elimu bora na malezi yanayostahili.
