Na Ashrack Miraji, Moshi

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, amewataka wananchi kuzingatia ulaji wa vyakula vya asili na kupunguza matumizi ya sukari, chumvi na mafuta mengi ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, yakiwamo kisukari na shinikizo la damu.

Mnzava ametoa wito huo Novemba 6, 2026, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa yaliyofanyika katika Hospitali ya St. Joseph, Manispaa ya Moshi, akisisitiza kuwa ulaji bora ni msingi wa afya njema kwa mtu mmoja mmoja, familia na jamii kwa ujumla.

Amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu isemayo “Imarisha Afya: Kula Kiasili, Punguza Sukari, Chumvi na Mafuta” inalenga kuhamasisha wananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu vyakula wanavyotumia kila siku ili kupunguza hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza.

Ameeleza kuwa takwimu za Halmashauri zinaonesha ongezeko la wagonjwa wa shinikizo la damu na kisukari kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo, hali inayohusishwa kwa kiasi kikubwa na ulaji usiofaa, matumizi ya vyakula vilivyosindikwa na vyenye sukari, chumvi na mafuta kwa wingi, pamoja na kutofanya mazoezi.

Kutokana na hali hiyo, amewataka wananchi kuzingatia mlo kamili unaojumuisha mboga za majani, matunda, nafaka, kunde na vyakula vyenye protini, huku akisisitiza umuhimu wa kufanya mazoezi mara kwa mara na kupima afya ili kubaini magonjwa mapema na kupata matibabu kwa wakati.

Aidha, amewataka wataalamu wa afya na lishe kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kwa lugha rahisi na kutumia mifano ya vyakula vinavyopatikana katika mazingira yao ili kuhakikisha elimu hiyo inafanyiwa kazi katika ngazi ya familia na jamii.