Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) kuimarisha ushiriki wa wanawake katika uongozi, maamuzi na michakato ya kuzuia na kutatua migogoro ili kujenga amani na usalama wa kudumu katika eneo hilo

Akizungumza leo Novemba 2,2026 wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Jukwaa la Wanawake wa Mabunge ya Ukanda wa Maziwa Makuu(WPC), unaofanyika Dar es Salaam, kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, Ndejembi amesema wanawake wana nafasi kubwa katika kujenga amani, kupatanisha jamii na kuimarisha maendeleo endelevu.

Amesema amani na usalama ni msingi wa maendeleo, hivyo nchi za ukanda huo hazipaswi kusubiri migogoro itokee ndipo zianze kutafuta suluhu, bali zinapaswa kuimarisha mifumo ya kuzuia migogoro na kulinda haki na usalama wa wananchi.

Amesema wanawake si wahanga wa migogoro pekee, bali pia ni viongozi, wapatanishi na wajenzi wa amani ambao mchango wao umekuwa muhimu katika kurejesha matumaini kwa jamii zilizoathiriwa na migogoro.

Ndejembi amesema licha ya hatua zilizopigwa, takwimu zinaonesha kuwa ushiriki wa wanawake bado ni mdogo, akibainisha kuwa kwa mujibu wa Umoja wa Mabunge Duniani, wanawake walikuwa na takribani asilimia 27.5 ya viti vya mabunge duniani hadi Januari mwaka 2026.

Ameongeza kuwa ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama ilionesha kuwa katika michakato mikuu ya amani iliyofanyika mwaka 2022, wanawake walikuwa asilimia saba tu ya washiriki katika majadiliano na asilimia 14 ya wapatanishi.

Amesema Tanzania inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake kushiriki katika uongozi na maendeleo, akitolea mfano Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo nchini, jambo linaloonesha kuwa wanawake wana uwezo wa kuongoza katika ngazi za juu.

Amebainisha kuwa Serikali pia imeendelea kuwaunganisha wanawake wajasiriamali na fursa za masoko, mitaji na mikopo yenye masharti nafuu, huku ikizindua Mpango wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama kwa kipindi cha mwaka 2025 hadi 2029.

Aidha, amesema Tanzania imeshiriki katika kuandaa mipango na mikakati ya kikanda ya ICGLR inayolenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika michakato ya amani, usalama, usuluhishi wa migogoro na utawala bora.

Katika hatua nyingine, Ndejembi ametoa mapendekezo matano kwa nchi wanachama, yakiwamo kuongeza ushiriki wa wanawake katika maamuzi, kuimarisha mitandao ya wanawake wapatanishi, kulinda wanawake na wasichana dhidi ya ukatili, kuwekeza kwa wanawake na vijana pamoja na kuimarisha ushirikiano na uwajibikaji wa kikanda.

Amesisitiza kuwa maazimio yatakayofikiwa katika mkutano huo yanapaswa kuambatana na mipango madhubuti ya utekelezaji, muda maalumu, taasisi zinazowajibika na viashiria vya kupima mafanikio ili kuhakikisha yanazaa matokeo kwa wananchi wa ukanda huo.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, amesema mkutano huo ni fursa muhimu ya kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikishwaji wa wanawake katika masuala ya amani, usalama na maendeleo.

Amesema Bunge la Tanzania linaendelea kuonesha dhamira ya kuwawezesha wanawake, akibainisha kuwa zaidi ya wabunge 39 ni wanawake na kamati saba za kudumu za Bunge zinaongozwa na wenyeviti wanawake.

Naye Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Judith Suminwa Tuluka, amesema ushiriki wa wanawake katika ujenzi wa amani haupaswi kuishia kwenye matamko na sheria, bali unahitaji hatua za vitendo, rasilimali na matokeo yanayoonekana.

Amesema wanawake na watoto katika maeneo ya mashariki mwa DRC wameendelea kukabiliwa na madhara ya migogoro, hivyo wanahitaji ulinzi, haki na nafasi ya kushiriki katika maamuzi yanayohusu mustakabali wa jamii zao.