Kigoma

Wananchi katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji wameeleza kunufaika na ujenzi wa Daraja la Luiche na kuepukana na adha walizokuwa wakipitia kipindi cha nyuma.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa TARURA Mkoa wa Kigoma Mhandisi Goodluck Mbanga kuwa TARURA kupitia Mradi wa Uendelezaji wa miundombinu ya miji Tanzania(TACTIC) waliamua kujenga Barabara ya Kagera- Wafipa yenye urefu wa Kilomita 1.45 kwa kiwango cha lami ikiwa ni sambamba na ujenzi wa daraja hilo la Luiche lenye urefu wa mita 36.

Kiongozi huyo amefafanua kuwa hapo awali wananchi walilazimika kutumia mitumbwi ili kuvuka na kuvusha mazao yao hali iliyopelekea kuhatarisha maisha yao.” Changamoto ilikuwa kubwa hasa katika kuvuka mto, wananchi walitumia mitumbwi ambapo hali ya usalama kwao ilikua mbaya lakini sasa wanavuka wakati wote bila matatizo”.Amesema Mhandisi Mbanga.

Naye, Bi. Ashura Ramadhani Mkazi wa Kata ya Kagera amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kunachangia katika kuinua uchumi wao kwani wanavuka muda wote bila kikwazo.” Ilikua kama ndoto maana hatukuamini kwamba ipo siku tutaepukana na kero za mitumbwi,kwa sasa mtu anavuka muda wote anaotaka, pia tumejengewa barabara nzuri ya lami kwakweli tunaipongeza Serikali kwa kazi hii nzuri” amesema Bi. Ashura. 

Aidha, Bw. Hussein Rajab ambaye pia ni mkazi wa Kata ya Kagera amesema kuwa mradi huo wa daraja pamoja na barabara umebadilisha maeneo yao nakwamba kwasasa kazi zinafanyika muda wote bila kikwazo tofauti na hapo awali.

” Mwanzoni tulitumia mitumbwi kuvuka hapa na tulikua tunalipia shilingi 200 lakini sasa tunavuka na vyombo vyetu vya usafiri kwa saa 24 hii tuliona kama ni ndoto lakini imewezekana.”Amesema Bw. Rajab.

Mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania unatekelezwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ambapo kupitia mradi huu miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara, masoko na stendi vinajengwa katika mikoa mbalimbali nchini.