‎Mpwapwa, Dodoma

‎Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Mhe. Dkt. Sophia Kizigo ameipongeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kuendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia Mpango wa Matengenezo ya Kawaida ya Barabara kwa Kutumia Vikundi vya kijamii (CBRM).

‎Amesema mpango huo si tu unachangia kuboresha na kutunza miundombinu ya barabara bali pia unafungua milango ya ajira, kuongeza kipato na kuimarisha uwezo wa wananchi kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli za uzalishaji.

‎Dkt. Kizigo ameyasema hayo leo tarehe 02 Novemba, 2026, wakati wa hafla ya kukabidhi mikataba 10 kwa vikundi 10 vya kijamii kutoka wilaya ya Mpwapwa iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.

‎Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Mpwapwa Mhandisi Emmanuel Lukumay amesema mikataba hiyo yenye thamani ya shilingi milioni 94 inahusisha vikundi vya kijamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kwa lengo la kuvipa nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika utekelezaji wa shughuli za matengenezo ya kawaida ya barabara kupitia mpango wa CBRM.

‎Ameeleza kuwa utekelezaji wa mikataba hiyo utawezesha vikundi kupata kipato kupitia kazi wanazozifanya huku ukijenga ujuzi, uzoefu na uwezo wa kusimamia shughuli za kiuchumi na biashara.

‎Akizungumza kwa niaba ya wanavikundi, Bi. Janet Makari ameishukuru TARURA kwa fursa hiyo akieleza kuwa itasaidia wanawake kupata kipato chao wenyewe, kujikwamua na changamoto za kiuchumi na kupunguza utegemezi wa mikopo yenye masharti magumu.

‎”Sisi kama wanawake tunashukuru kwa kupata fursa hii kwani kazi hii itatusaidia kufanya kazi na kupata kipato chetu wenyewe ili tuweze kujiendeleza kiuchumi badala ya kutetemea mikopo yenye masharti magumu”, amesema Bi. Makari.

‎Mikataba hiyo imeanza kutekelezwa rasmi leo na itadumu kwa kipindi cha mwaka mmoja na TARURA itavipatia vikundi hivyo vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa kazi pamoja na mavazi maalumu ya kujikinga na kujitambulisha wanapokuwa kazini.

‎Sambamba na hilo, TARURA inaendelea kushirikiana na Afisa Biashara wa wilaya pamoja na wadau wa taasisi za kifedha kutoa elimu na ushauri kuhusu usimamizi wa fedha, biashara na uwekezaji ili kuhakikisha vikundi hivyo vinatumia fursa hiyo kama chachu ya kukuza mitaji, kuanzisha shughuli nyingine za kiuchumi na kujenga ustawi wa muda mrefu.