Na.Sophia Kingimali.

Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza uamuzi wa Tanzania kufungua tena ubalozi wake nchini Angola, huku nchi hizo zikikubaliana kuunganisha reli ya TAZARA na Benguela ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kukuza biashara kati ya mataifa hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Octoba 29,2026 baada ya mazungumzo rasmi na Rais wa Angola, João Lourenço, yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema hatua hizo zinalenga kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kutumia fursa zilizopo katika biashara na uwekezaji.

Amesema pamoja na uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Angola, biashara kati ya nchi hizo bado ni ndogo, hivyo wamekubaliana kuandaa kongamano la biashara na uwekezaji litakalowakutanisha wafanyabiashara na sekta binafsi kutafuta maeneo ya kushirikiana.

Rais Samia amesema Tanzania imeamua kufungua tena ubalozi wake nchini Angola na kwamba atateua balozi hivi karibuni ili kurahisisha mawasiliano, kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kuongeza fursa za kiuchumi kati ya mataifa hayo.

Kuhusu miundombinu ya usafirishaji, amesema nchi hizo zimekubaliana kuendeleza uunganishaji wa reli ya TAZARA na reli ya Benguela, hatua itakayowezesha bidhaa kusafirishwa kutoka Bandari ya Dar es Salaam katika Bahari ya Hindi hadi Bandari ya Lobito nchini Angola katika Bahari ya Atlantiki.

Amesema pia Tanzania na Angola zimesaini makubaliano ya huduma za usafiri wa anga yatakayoweka mazingira ya kuanzishwa kwa safari za moja kwa moja, kupunguza usumbufu wa safari na kuchochea biashara, uwekezaji na utalii kati ya nchi hizo.

Katika sekta ya nishati, Rais Samia amesema Angola imeikaribisha Tanzania kushirikiana katika shughuli za usafishaji wa mafuta, huku Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) likianza kuchunguza uwezekano wa kuingia ubia katika mradi wa mafuta wa Lobito.

Ameongeza kuwa nchi hizo zimekubaliana kushirikiana katika sekta ya madini kwa kubadilishana uzoefu, kujenga uwezo wa wachimbaji wadogo na wataalamu pamoja na kuongeza thamani ya madini ili kunufaisha uchumi wa mataifa hayo.

Kwa upande wake, Rais Lourenço amesema kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kutazalisha fursa za maendeleo kwa wananchi wa Tanzania na Angola, akisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kushirikiana badala ya kutegemea zaidi uhusiano na mataifa ya Ulaya, Amerika na Asia.

Amesema kuunganisha reli za TAZARA na Benguela ni mradi muhimu utakaounganisha bandari za Dar es Salaam na Lobito, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kufungua njia mpya za biashara kati ya nchi hizo na maeneo mengine ya bara la Afrika.

Rais Lourenço ameeleza kuwa Angola pia iko tayari kushirikiana na Tanzania katika matumizi ya satelaiti yake ya Angosat-2 kwa maendeleo ya teknolojia, ufuatiliaji wa hali ya hewa na shughuli nyingine za kiuchumi, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika elimu na afya.

Aidha, viongozi hao walijadili masuala ya amani na usalama katika ukanda wa Kusini mwa Afrika na Maziwa Makuu, hususan mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), pamoja na kuunga mkono mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kuongeza uwakilishi wa Afrika na maeneo mengine duniani.

Awali, Tanzania na Angola zilisaini mikataba mitatu na hati za makubaliano zinazohusu kubadilishana watu waliohukumiwa, huduma za usafiri wa anga, mawasiliano na ushirikiano katika masuala ya hali ya hewa kati ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na taasisi husika ya Angola.

Uhusiano wa Tanzania na Angola ulijengwa na viongozi waasisi wa mataifa hayo, akiwemo Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Dkt. António Agostinho Neto, walioshirikiana katika harakati za ukombozi wa Afrika. Ziara hiyo inalenga kuendeleza urafiki huo wa kihistoria kwa kuimarisha biashara, uwekezaji na maendeleo ya wananchi wa nchi hizo mbili.