Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Nsubili Joshua, akiongoza kikao cha Maafisa Masuhuli wanaohusika na ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, kilichofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Nsubili Joshua (katikati), akisisitiza umuhimu wa Wizara, Taasisi na Mashirika ya Umma yanayokusanya mapato yasiyo ya kodi kutumia kikamilifu fursa zilizopo ili kuongeza mapato ya ndani wakati wa kikao na Maafisa Masuhuli wanaohusika na ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi kilichofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square. Kushoto ni Kaimu Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha, Mhandisi Kenneth Nindie na kulia ni Kamisha Msaidizi Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha Bw. William Mhoja.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Agnes Meena na Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa wizara hiyo Bi. Eleonora Saitoria wakifuatilia majadiliano wakati wa kikao cha Maafisa Masuuli wanaohusika na ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi, kilichofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square.

Kamisha Msaidizi Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha Bw. William Mhoja akiwasilisha maelezo kuhusu mwenendo wa ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi wakati wa kikao cha Maafisa Masuhuli wanaohusika na ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi, kilichofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square.

Manaibu Kamishna wa Idara ya uchambuzi wa Sera Wizara ya Fedha Bw. Juma Mkabakuli (Kushoto) na Dkt. Iddy Kayumba wakifuatilia majadiliano wakati wa kikao cha Maafisa Masuuli wanaohusika na ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi, kilichofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square.

Mchumi, Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha Bi. Jenipher Rauya akitoa wasilisho kuhusu mwenendo wa mapato yasiyo ya kodi, wakati wa wakati wa kikao cha Maafisa Masuuli wanaohusika na ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi, kilichofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square.

Afisa Usimamizi wa Fedha Mkuu, Idara ya Uchambuzi wa Sera Bi. Emerensiana Nyanda, akifanya wasilisho kuhusu mrejesho wa utekelezaji wa maazimio yatokanayo na kikao cha Maafisa Masuuli kilichofanyika Septemba 2025/206, wakati wa kikao cha Maafisa Masuuli wanaohusika na ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi, kilichofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha Bw. Nsubili Joshua, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Maafisa Masuuli, wanaohusika na ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi, baada ya kumalizikia kwa kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Kambarage,

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)

……………….. 

Na Joseph Mahumi, Zanzibar

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amewataka wahitimu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Zanzibar kuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya umma na binafsi nchini kupitia taaluma waliyoipata.

Akizungumza katika Mahafali ya kwanza ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania Kampasi ya Zanzibar, Mhe. Balozi Omar alisisitiza kuwa wahitimu hao wanapaswa kuwa suluhu ya kweli katika utekelezaji wa Dira 2050 huku akibainisha kuwa sekta binafsi ina kazi kubwa ya kutekeleza asilimia 70 ya Dira hiyo.

Aliwahimiza kutokuwa wataalamu wa kulalamika, bali wawe wabunifu na watatuzi wa changamoto kwa kutumia teknolojia na kuwa waadilifu.

“Nawapongeza TIA Kampasi ya Zanzibar kwa kupiga hatua kubwa katika kutoa elimu bora pamoja na kuzingatia masuala ya kijinsia kwa kuwa mmekuwa mkidahili wanafunzi wengi wanawake” alisema Balozi Omar

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu – TIA, Prof. William Pallangyo, alisema jumla ya wanafunzi 188 wamehitimu katika Kampasi hiyo kwa mwaka huu, idadi ambayo ni asilimia 1.3 ya wahitimu wote wa TIA nchi nzima zaidi ya elfu 34.

Alisema kati ya wahitimu hao, wanawake ni 127 sawa na asilimia 67.5, jambo ambalo linaashiria utekelezaji wa Dira 2050 inayosisitiza usawa wa kijinsia na uwekezaji kwa wanawake kama injini ya maendeleo.

Aidha, wahitimu 123 ni wa ngazi ya uzamili, huku 65 wakiwa ni wa ngazi ya cheti na cheti cha awali.

Akizungumzia Mradi wa Ujenzi wa Kampasi ya kudumu ya TIA unaoendelea katika eneo la Makunduchi-mjini Unguja, unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Fedha, alisema mradi huo umefikia asilimia 45 ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ambapo hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi bilioni 15.9.

“Mradi utakapo kamilika unatarajiwa kuongeza uwezo wa chuo kudahili kutoka wanafunzi 267 hadi kufikia 1,704 pindi utakapokamilika” alisema Prof. Pallangyo

Aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ufadhili wa ujenzi huo, pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kutoa eneo la ekari 60 kwa ajili ya ujenzi wa Kampasi hiyo.

Prof. Palangyo amesema katika kuimarisha taaluma, TIA Zanzibar imeingia makubaliano ya ushirikiano na vyuo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi, ikiwemo Chuo Kikuu cha Eduardo Mondlane na Chuo Kikuu cha Rovuma kutoka Msumbiji, na ushirikiano huo unalenga kubadilishana wanafunzi na kuimarisha tafiti na mafunzo.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Wizara ya Fedha wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Prof. Jehovaness Aikael, alisema kuwa TIA ina jukumu muhimu la kuwa kinara wa elimu katika fani za uhasibu, ugavi, biashara na taaluma nyingine zinazochangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, hivyo kuna umuhimu wa kuandaa wataalamu wenye maarifa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko na uwekezaji.

Alisema Bodi ya Ushauri itaendelea kuhakikisha kuwa mitaala ya TIA inaendana na mahitaji ya soko la ajira, mabadiliko ya teknolojia na vipaumbele vya maendeleo ya taifa, hususan matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), uhasibu unaozingatia viwango vya kimataifa na uchumi wa buluu, ili wahitimu waweze kutumia taaluma zao kutatua changamoto za maendeleo badala ya kutoa elimu ya nadharia pekee.

“Bodi itasimamia matumizi sahihi ya rasilimali zinazotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya elimu na kuongeza uwezo wa taasisi kutoa mafunzo bora” alisema Prof. Aikael.

Aliongeza kuwa TIA Kampasi ya Zanzibar inalenga kuwa kitovu cha umahiri katika uchumi wa buluu kupitia ushirikiano na taasisi nyingine za elimu na kitaaluma, zikiwemo Chuo cha Utawala wa Umma, Taasisi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu pamoja na Chuo cha Mafunzo ya Sayansi na ushirikiano huo utasaidia kuimarisha ubora wa elimu, kubadilishana ujuzi na uzoefu, na kuhakikisha wataalamu wanaozalishwa wanakidhi viwango vya kimataifa na kuwa na uwezo wa kuchochea maendeleo endelevu ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) ni taasisi ya Serikali inayomilikiwa na Wizara ya Fedha ikiwa ina jumla ya Kampasi 8 zilizoko katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Mbeya, Zanzibar, Singida, Dodoma, Mtwara na Dodoma.