Na Mwandishi wetu, Mirerani

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeelezwa kuwa gramu 274,634.32 za madini ya Tanzanite za thamani ya Sh3.23 bilioni zimezalishwa kwa miezi mitatu ya robo ya kwanza ya mwaka kuanzia mwezi Julai hadi Septemba 2026.

Ofisa madini mkazi wa mkoa wa kimadini wa Mirerani, (RMO) George Kaseza, ameeleza hayo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilipotembelea maeneo ya machimbo ya madini ya Tanzanite.

Kaseza amesema katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027, kuanzia Julai hadi Septemba 2026, jumla ya gramu 274,634.32 za Tanzanite zilizalishwa, zikiwa na thamani ya Sh3.23 bilioni.

Amesema uzalishaji wa Tanzanite Beads ulikuwa gramu 8,622,049.36 zenye thamani ya Sh95.83 milioni huku Tanzanite Clive ikiwa na uzito wa gramu 20,562.35 na thamani ya Sh16.73 milioni.

Amesema ujenzi wa Ukuta wa Mirerani uliokamilika Aprili 2018 na kuanzishwa kwa soko la madini Mirerani mwaka 2021 na eneo hilo lina kamera za usalama (CCTV) 310 na taa 573, huku mwaka 2026 Serikali ikiagiza kofia ngumu 12 zenye kamera kwa ajili ya wadhibiti wa madini chini ya migodi.

Amesema kuhusu biashara ya Tanzanite, katika mwaka wa fedha 2025/2026, mnada wa wafanyabiashara wadogo uliofanyika Mei 15, 2026, uliwezesha kuuzwa kwa gramu 2,809.31 za Tanzanite zenye thamani ya Sh271.270 bilioni huku mnada wa wafanyabiashara wakubwa uliofanyika Mei 21, 2026, ukiwezesha kuuzwa kwa gramu 10,174.92 zenye thamani ya Sh721.750 bilioni.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Subira Mgalu amesema ziara hiyo imelenga kujifunza na kutathmini shughuli za uchimbaji, biashara na uongezaji thamani wa madini zinazofanyika ndani ya ukuta wa Mirerani.

Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara, (MAREMA) Elisha Mnyawi ametoa ombi la lango la kuingilia na kutoka ndani ya ukuta wa madini ya Tanzanite lifanye kazi saa 24 kwani hivi sasa ikifika saa 12 jioni wachimbaji hawaruhusiwi kuingiza zana za kazi.

Mwenyekiti wa MAREMA Tawi la Mirerani, Samwel Rugemalila, ameishukuru Serikali kwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa kuboresha sekta hiyo. 

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Madini ndani ya Ukuta wa Mirerani, Magreth Nelson, ameishukuru Serikali kwa kurejesha mnada wa madini, akisema hatua hiyo imewawezesha wafanyabiashara kuuza madini yao kwa uwazi na katika mazingira ya ushindani wa bei.

Mjumbe wa chama cha wafanyabiashara wa madini Victor Kunyara ametoa ombi kwa kamati hiyo kuweka kanuni kwa wachimbaji madini watenge asilimia 10 ya uzalishaji wa madini wawauzie ili wafanyabiashara wapate kipato na kulipa kodi.