Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, ameshiriki Site Trust Nishati Safi Marathon 2026 iliyofanyika leo, Oktoba 24, 2026, katika Wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma, kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuchangisha fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo.
Kupitia marathon hiyo, jumla ya shilingi milioni 102 zimekusanywa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vitakavyosaidia kuboresha huduma za matibabu na kuongeza uwezo wa hospitali hiyo kuwahudumia wananchi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Homera amesema Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034, unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034. Amesisitiza kuwa matumizi ya nishati safi yatasaidia kulinda afya za wananchi na kuhifadhi mazingira.
Aidha, amezipongeza TANESCO, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) pamoja na wadau wengine kwa kushiriki katika kufanikisha marathon hiyo na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Katika kuendeleza juhudi hizo, REA imetoa majiko 1,000 ya nishati safi, yakiwemo majiko yanayotumia gesi, majiko banifu na majiko ya umeme, ili kuongeza uelewa na kuhamasisha wananchi kutumia teknolojia hizo.
Akiwa ametembelea mabanda ya TANESCO na REA katika viwanja vya marathon hiyo, Dkt. Homera amezitaka taasisi hizo kuandaa mikakati ya kuongeza matumizi ya nishati safi nchini, ikiwemo kuanzisha mifumo ya malipo ya awamu inayowawezesha wananchi kupata teknolojia za nishati safi kwa gharama nafuu.

