Serikali ya Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro inatarajia kuanza operesheni maalumu ya siku saba kuanzia Oktoba 26, 2026 ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu, hususan tembo wanaoingia katika maeneo ya makazi na shughuli za kibinadamu ikiwemo mashamba.

Operesheni hiyo itatekelezwa kwa ushirikiano na taasisi za uhifadhi zilizopo wilayani humo, ambazo ni Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Akizungumza kuhusu operesheni hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, amesema kuwa operesheni hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati iliyowekwa na Serikali kwa kushirikiana na taasisi hizo ili kupunguza changamoto ya wanyamapori hao kuingia katika maeneo ya makazi na shughuli za kibinadamu ambapo hatua hiyo inalenga kuimarisha usalama wa wananchi na kuwawezesha kufanya shughuli zao za kila siku bila hofu.

Amesema kuwa tayari taasisi hizo zimeandaa vikosi vinne vitakavyotekeleza operesheni hiyo kwa siku saba kuanzia Jumatatu, Oktoba 26, 2026, kwa lengo la kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu, hususan tembo, wanaoingia katika maeneo ya wananchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Eva Mallya, amesema operesheni hiyo itatekelezwa kwa umakini mkubwa kwa kushirikiana na wananchi wa maeneo lengwa, amewasisitiza wananchi kutoa ushirikiano kwa vikosi hivyo ili kufanikisha zoezi hilo na kupunguza migongano kati ya binadamu na wanyamapori.

Naye Kamanda anayesimamia Mapori Tengefu ya Ruvu-Same, Karimawe na Mto Umba kutoka TAWA, Lackson Mwamwezi, amesema vikosi hivyo vitasambazwa katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Same. Kikosi cha kwanza kitakuwa Kata ya Maore kikihudumia Maore, Kisiwani na Ndungu, kikosi cha pili kitahudumia Kata za Makanya na Hedaru, kikosi cha tatu kitakuwa Kata ya Njoro, na kikosi cha nne kitakuwa Kata ya Ruvu.

Aidha, operesheni hiyo itaambatana na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na kukabiliana na hatari zinazoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu. Amewataka wananchi kushirikiana na vikosi hivyo vitakapofika katika maeneo yao ili kufanikisha utekelezaji wa operesheni hiyo.