Na. Mwandishi Maalum

24/10/2026 Wanamichezo wa ngumi za kulipwa nchini wametakiwa kupima moyo kabla ya kuingia ulingoni ili kubaini mapema changamoto zinazoweza kuhatarisha maisha yao wakati ama baada ya michezo.

Rai hiyo imetolewa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Eva Wakuganda wakati wa kambi maalumu ya siku tatu ya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wanamichezo wa ngumi za kulipwa Tanzania inayofanyika katika viwanja vya Mafia Boxing Sports Promotion Magomeni jijini Dar es Salaam.

Dkt. Eva ambaye pia ni Mratibu wa Magonjwa ya Moyo kwa Wanamichezo alisema uchunguzi wa moyo kwa mabondia ni muhimu kwa sababu wanaweza kujiona kuwa na afya njema kwa nje kumbe wanamatatizo ya moyo ambayo yanaweza kukatisha uhai wao wawapo michezoni.

“Tunataka wanamichezo wote wafanye mazoezi yaliyo salama, mtu anapofanya mazoezi anaweza akajiona kwamba yuko vizuri kumbe na changamoto mbalimbali kwa hiyo kabla ya kufanya mazoezi ni lazima ufanye vipimo vya moyo kuangalia kama uko vizuri”, alisema Dkt. Eva.

Dkt. Eva aliongeza kuwa mabondia hawapaswi kusubiri mpaka wajisikie wagonjwa ndipo watafute huduma za afya bali wanapaswa kufanya uchunguzi wa mara kwa mara ili kubaini mapema changamoto zinazoweza kuathiri afya zao na uwezo wao wa kuendelea na mchezo.

“Ni muhimu mwanamichezo wakafanyiwa vipimo vya moyo kabla ya kuanza mazoezi na wakaendelea kufuatiliwa afya zao mara kwa mara lengo ni kuhakikisha wanafanya mazoezi na kushiriki mashindano wakiwa salama”, alisema Dkt. Eva.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) Jacob Mbuya alisema ngumi ni mchezo unaohitaji umakini mkubwa katika masuala ya afya na usalama wa mabondia hivyo fursa ya kufanyiwa uchunguzi wa afya kupitia ushirikiano na JKCI ni muhimu kwa ustawi wa wanamichezo hao.

“Mchezo halisi ni mchezo wa boxing ambao unahesabika kuwa mchezo hatari namba moja duniani hivyo basi kama ni mchezo hatari lazima kutakuwa na athari kubwa zinazoweza kuwapata mabondia, tumefurahi tumepata fursa ya kipekee ya kupata huduma za uchunguzi wa afya kutoka kwa ndugu zetu wa JKCI”, alisema Mbuya.

Kwa upande wake bondia kutoka Mafia Boxing Sebastian Deo amesema alisema imekuwa siku ya furaha kwake kupata huduma za uchunguzi wa afya huku akiomba huduma hizo ziendelee kutolewa mara kwa mara ili mabondia wengi zaidi wanufaike.

“Changamoto za moyo na maradhi mengine ni jambo ambalo limekuwa likitushangaza, hii ni huduma nzuri naomba isiishie hapa waendelee kutufanyia uchunguzi sisi mabondia tutajitokeza ili tuendelee kuchunguza afya zetu na kuwa bora tunapoingia ulingoni”, alisema Sebastian.