DODOMA
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezindua Mkakati wa Kitaifa wa Elimu Jumuishi wa mwaka 2026/2027 hadi 2030/2031 pamoja na miongozo tisa ya utekelezaji wake, huku ikitoa vifaa saidizi vyenye thamani ya Sh milioni 730 kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu katika shule za sekondari na vyuo vikuu nchini.
Hatua hiyo inalenga kuondoa vikwazo vya kielimu, kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji na kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wanapata fursa sawa za elimu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika leo Oktoba 16,2026 jijini Dodoma,Waziri wa wizara hiyo Profesa Adolf Mkenda,amesema serikali inaendelea kuimarisha elimu jumuishi ili kila mtoto apate nafasi ya kujifunza na kuendeleza uwezo wake bila kujali hali yake ya kimwili. Alisema utekelezaji wa mkakati huo unahitaji ushirikiano wa serikali, Bunge, wadau wa maendeleo, walimu na wazazi ili kuhakikisha haki ya elimu inafikiwa kwa vitendo.
Profesa Mkenda amesema serikali imewekeza zaidi ya Sh bilioni 12 katika kuboresha miundombinu ya elimu maalum na jumuishi, ikiwemo shule jumuishi za mfano na shule kongwe za elimu maalum.
Aidha, watumishi 2,058 wamepatiwa mafunzo, wakiwemo walimu wa elimu maalum 1,276, walimu wenye ulemavu 242 na Walezi na mawadeni 316. Serikali pia imechapisha na kusambaza vitabu 522,600 vya Breli na vitabu 850,000 vyenye maandishi yaliyokuzwa kwa wanafunzi wasioona na wenye uoni hafifu.
“Mafunzo ya Lugha ya Alama ya Tanzania yamefanywa kuwa ya lazima kwa walimu tarajali nchini ili kuwawezesha kuwasiliana na kufundisha wanafunzi viziwi kwa ufanisi”amesema Profesa Mkenda
Hata hivyo ameongeza kuwa serikali imeendelea kupanua mafunzo ya elimu maalum na jumuishi, ikiwemo kutoa ufadhili kwa walimu tarajali 2,000 wanaosoma shahada ya elimu maalum, huku vyuo vinavyotoa mafunzo hayo vikiongezeka kutoka kimoja hadi vitatu, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa katika hafla hiyo.
Profesa Mkenda, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuacha kuwaficha watoto wenye ulemavu na badala yake kuwaandikisha katika taasisi zinazokidhi mahitaji yao, akisisitiza kuwa unyanyapaa na mitazamo hasi haipaswi kuwanyima watoto hao haki ya elimu.
“Serikali itaendelea kushirikiana na wazazi kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kujifunza bila kujali aina au ukubwa wa ulemavu wake, huku akizitaka jamii na taasisi za elimu kuimarisha mazingira rafiki kwa wanafunzi hao.”amesisitiza
Aidha, Profesa Mkenda amezitaka taasisi za elimu, wadau wa maendeleo, mashirika ya dini na sekta binafsi kuendelea kushirikiana na serikali katika kutoa vifaa saidizi, mafunzo na huduma zinazohitajika.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya mkakati huo hayatapimwa kwa idadi ya miongozo iliyozinduliwa au vifaa vilivyogawiwa pekee, bali kwa matokeo halisi katika kuboresha mazingira ya kujifunzia, ushiriki wa wanafunzi na kiwango cha elimu wanachopata, hatua inayotarajiwa kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Katika hatua nyingine, Serikali imeanzisha programu za shule nyumbani na shule za hospital kwa wanafunzi wasioweza kuhudhuria masomo katika madarasa ya kawaida kutoka na na hali zao za kiafya ikiwemo 691 wanaosoma shule nyumbani na wanafunzi 60 walioko katika hospitali mbalimbali nchini
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko, amewataka wanafunzi wenye ulemavu kutovunjika moyo, akisisitiza kuwa ulemavu si kikwazo cha kutimiza ndoto na malengo yao.
Sekiboko ametumia mfano wa Mbunge Yumna, ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo, kueleza namna watu wenye ulemavu wanavyoweza kushiriki katika uongozi na kutoa mchango mkubwa kwa taifa.
Amesema Yumna amekuwa mstari wa mbele kuwasemea watu wenye ulemavu katika vikao vya Bunge na kamati, akieleza kuwa wanafunzi wakitumia vifaa saidizi kwa usahihi, kuweka juhudi katika masomo na kujiamini, wanaweza kufikia mafanikio makubwa kama viongozi wengine nchini.
“Mheshimiwa Yumna ni mbunge na mjumbe mwenye hoja nzuri anayejua kuelezea mambo na anawasemea sana watu wenye ulemavu. Ninaamini mkiandamana, mkatumia vifaa hivi kwa usahihi, mkaweka juhudi na kujipanga kusoma, katika nchi hii tutakuwa na akina Yumna wengi wa kutosha mnaoweza kuleta mchango mkubwa kwa taifa,” amesema Sekiboko.
Ameitaka Wizara ya Elimu kuhakikisha mpango wa utoaji wa vifaa saidizi unaendelea na kuwafikia wanafunzi wengi zaidi katika mikoa yote nchini, huku akiahidi kuwa Bunge litaendelea kuunga mkono juhudi hizo kupitia usimamizi na utengaji wa bajeti zinazolenga kutatua changamoto za elimu jumuishi.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, amesema Serikali imeendelea kutekeleza hatua za kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma katika kupata haki ya elimu, akibainisha kuwa ugawaji wa vifaa saidizi uliofanyika ni mara ya tatu katika mwaka huu wa kalenda.
Profesa Nombo amewashukuru viongozi wa Serikali na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kwa ushirikiano wao katika kuimarisha sekta hiyo, huku akimtambua Mkurugenzi wa Elimu Maalumu wa wizara hiyo, Dk. Matonya, kwa kuratibu na kusimamia masuala ya elimu maalumu kuanzia ngazi ya awali hadi nje ya mfumo rasmi.
Awali Mwakilishi wa UNICEF,Ayubu Kafikilo,amesema kupitia ufadhili wa Serikali ya Canada, UNICEF imetoa kompyuta mpakato 200 na tableti 240 kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wenye ulemavu kunufaika na teknolojia ya kidijitali katika ujifunzaji.
Shirika hilo pia linaendelea na maandalizi ya upatikanaji wa vifaa vingine saidizi, vikiwemo vifaa vya nukta nundu, vifaa vya kusaidia kusikia, magongo na viti vya magurudumu ili kuongeza uwezo wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu kushiriki katika shughuli za elimu.
Aidha, UNICEF inashirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kubadilisha vitabu vya kawaida vya mtaala kuwa vitabu vya kidijitali vinavyoweza kutumiwa na wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ikiwemo mifumo ya unganisho na akili bandia.
UNICEF imepongeza hatua ya Serikali kujumuisha vitabu hivyo vya kidijitali katika Mkakati wa Kitaifa wa Elimu Jumuishi, ikisisitiza kuwa elimu jumuishi haiishii katika kuhakikisha watoto wanapata nafasi ya kujiunga na shule, bali pia inahusisha kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika masomo, wanapata ujuzi na kufikia uwezo wao.
Mkakati huo pamoja na miongozo tisa iliyozinduliwa unahusisha maeneo mbalimbali, ikiwemo mafunzo kwa walimu, matumizi ya TEHAMA na teknolojia saidizi, Lugha ya Alama ya Tanzania, elimu ya amali, huduma kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na matumizi ya Breli ya Kiswahili.

