NA DENIS MLOWE, MVOMERO

MKUU wa Wilaya ya Mvomero, Richard Kasesela, ametembelea eneo lililoathiriwa na mafuriko katika Kijiji cha Kichangani, Kata ya Mhonda na kuagiza kuchukuliwa kwa hatua za dharura ili kuzuia athari zaidi kabla mvua za El NiƱo hazijaanza.

Katika ziara hiyo iliyolenga kukagua maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko pamoja na mto Dc Kasesela amewashauri viongozi na wananchi kushirikiana katika juhudi za awali, ikiwa ni pamoja na kujaza vifusi kwenye mifuko na kuweka kwenye kingo za mto huo ili kupunguza nguvu ya maji pindi mvua zitakaponyesha.

Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho Kasesela wa alisema kuwa Serikali imeshaandaa mikakati ya kudumu ya kutatua changamoto hiyo ikiwemo mpango wa muda mrefu unahusisha ujenzi wa mabwawa mawili makubwa ambayo yatasaidia kupunguza kasi ya maji ya mto huo, ambayo mara nyingi huambatana na mchanga mwingi unaosababisha mto kujaa na kufurika.

Mbali na ujenzi wa mabwawa ameongeza kuwa Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri tayari imewasilisha maombi ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa kingo imara za mto huo ili kumaliza kabisa kero hiyo ya muda mrefu.

Aidha DC Kasesela pia amewataka wananchi kuwa wavumilivu wakati serikali ikiendelea kutatua changamoto zilizopo na kuwataka kuendelea kuchukua tahadhari katika kipindi hiki ambapo kunatarajiwa kuwa na mvua za El nino.

Nao miongoni mwa wananchi walioathirika na mafuriko hayo akiwemo Mchungaji Makundi ameeleza kuwa mafuriko hayo yameanza mwezi Februari mwaka huu ambapo yaliathiri mali zikiwemo makazi, mashamba, mifugo na miundombinu nyingine huku wananchi walioathirika wakihamishiwa kwenye makambi na wengine wakihifadhiwa na ndugu, jamaa na marafiki.