PRETORIA, AFRIKA KUSINI
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Mawaziri wa Ushirikiano wa Nchi Tatu za Tanzania, Msumbiji na Afrika Kusini, unaolenga kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu unaovuka mipaka.
Mkutano huo umefanyika jana, Oktoba 15, 2026, jijini Pretoria, Afrika Kusini, ukitanguliwa na kikao cha viongozi waandamizi kilichofanyika Oktoba 14, mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano huo, Profesa Kabudi amezitaka nchi hizo kuimarisha ushirikiano kwa kubadilishana taarifa za kiintelijensia ili kuwabaini wahalifu, kuvunja mitandao yao na kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka.
“Lengo la mkutano huo lilikuwa kujadili mikakati ya kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo katika kudhibiti usafirishaji haramu wa dawa za kulevya katika ukanda wa Bahari ya Hindi, pamoja na uhalifu mwingine unaojumuisha usafirishaji haramu wa binadamu, utekaji nyara na uhalifu wa kuvuka mipaka”amesema Profesa Kabudi
Amesema kuwa ushirikiano wa karibu kati ya vyombo vya usalama ni muhimu katika kudhibiti vitendo vya uhalifu vinavyotumia mianya ya mipaka na udhaifu wa mifumo ya udhibiti kutekeleza shughuli haramu.
Katika hatua nyingine, Profesa Kabudi amewakaribisha rasmi wanachama wa TPC nchini Tanzania, ambayo kwa kushirikiana na Kenya na Uganda inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika Juni na Julai 2027.
Alisisitiza nchi hizo kutumia fursa ya mashindano hayo kuimarisha mikakati ya kupambana na dawa za kulevya na uhalifu mwingine, akieleza kuwa matukio makubwa ya kimataifa yanaweza kutumiwa na wahalifu kutekeleza shughuli zao haramu.
Aidha, mkutano huo uliridhia maombi ya Angola na Uganda kujiunga na TPC, ambayo makao makuu yake yako nchini Msumbiji.
Kwa hatua hiyo, umoja huo sasa unaundwa na nchi tano ambazo ni Afrika Kusini, Angola, Msumbiji, Tanzania na Uganda, hatua inayotarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka.
Mkutano huo uliwakutanisha pia viongozi waandamizi kutoka mamlaka za kudhibiti dawa za kulevya, vyombo vya polisi na wadau wa maendeleo, wakiwemo Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) na Umoja wa Ulaya.
Washiriki kutoka Angola, Uganda, Comoro, Shelisheli, Eswatini, Uingereza na Marekani pia walishiriki majadiliano kuhusu namna bora ya kukabiliana na changamoto za uhalifu, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.

