Ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mlima Kilimanjaro (MK-ICC) jijini Arusha, unaogharimu Shilingi bilioni 398.92, unalenga kuimarisha nafasi ya Tanzania katika utalii wa mikutano, makongamano, maonesho na matukio makubwa ya kimataifa, pamoja na kuchochea uwekezaji na ukuaji wa uchumi.

 Hayo yameelezwa jijini Dodoma Oktoba 16, 2026 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Bw. Charles Kadonya wakati akiwasilisha taarifa ya Wizara yake kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) 2026 chini ya Mwenyekiti wake, Mhe. Najma Giga.

Alisema mradi huo wa kimkakati unatekelezwa kupitia ubia kati ya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), katika eneo la Kijenge lenye ukubwa wa takribani ekari 48.2. Katika ubia huo, AICC inachangia ardhi huku PSSSF ikigharamia ujenzi.

Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa mradi, mkataba wa ujenzi ulisainiwa Desemba 15, 2025, kati ya AICC, PSSSF na mkandarasi China Railway Construction Engineering Group (CRCEG), huku kampuni ya Dar Al-Handasah Consultants (Shair and Partners) ikiwa mshauri mwelekezi wa mradi.

Bw. Kadonya aliwaeleza wajumbe wa NUU kuwa ujenzi ulianza rasmi Januari 12, 2026, baada ya eneo la mradi kukabidhiwa kwa mkandarasi Desemba 22, 2025. Mradi umepangwa kutekelezwa kwa siku 540 na unatarajiwa kukamilika Julai 5, 2027, kisha kufuatiwa na kipindi cha uangalizi wa miezi 12.

Kituo hicho kitakuwa na ukumbi mkuu wa mikutano wenye uwezo wa kuhudumia washiriki 5,000 kwa wakati mmoja, kumbi ndogo za mikutano zitakazohudumia watu kati ya 30 na 500, ukumbi wa hadhi ya viongozi wakuu wenye uwezo wa watu 300, pamoja na ukumbi wa maonesho wenye eneo la mita za mraba 20,000 na uwezo wa kuhudumia washiriki 10,000.

Manufaa yanayotarajiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wageni wa kimataifa, mapato ya fedha za kigeni na mapato ya Serikali, pamoja na kutengeneza ajira wakati na baada ya ujenzi. Aidha, mradi unatarajiwa kuchochea shughuli za hoteli, usafiri, huduma za chakula, usalama na biashara nyingine, huku ukiimarisha taswira ya Tanzania kama kituo cha mikutano ya kimataifa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Wajumbe wa NUU kwa upande wao walisisitiza umuhimu wa kuimarisha miundombinu wezeshi kama vile barabara, madaraja, umeme, TEHAMA ili kituo hicho ambacho ni maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kiweze kuwa na manufaa yanayokusudiwa.