Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma 

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imeipongeza Hospitali ya Kanda ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa juhudi inazofanya katika kutoa huduma za afya, huku ikiitaka hospitali hiyo kuendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa.Pongezi hizo zimetolewa Oktoba 15, 2026 na Naibu Kamishna wa TIRA, Khadija Said, wakati akiongoza ziara katika Hospitali ya Benjamin Mkapa ( BMH ), ambapo TIRA pamoja na wadau wake wa bima walitoa msaada kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za hospitali katika kuendeleza huduma za afya kwa watoto.

Huku akibainisha Kuwa TIRA inatambua kazi kubwa inayofanywa na madaktari wa upasuaji na wataalamu wengine wa afya wanaowahudumia watoto, akiwapongeza kwa weledi, kujituma na moyo wa huruma wanaouonesha katika kuwahudumia wagonjwa.

Amebainisha kuwa yeye binafsi ameshuhudia namna madaktari wanavyoguswa na hali za wagonjwa, Aidha, Khadija amesema TIRA pamoja na kutekeleza jukumu lake la kusimamia na kuendeleza sekta ya bima nchini, inatambua umuhimu wa bima katika kusaidia wananchi kukabiliana na athari za kifedha zinazoweza kusababishwa na majanga mbalimbali ikiwemo changamoto za kiafya.

Amesema bima ni nyenzo muhimu ya ulinzi wa kifedha inayoweza kusaidia watu binafsi, familia na taasisi kukabiliana na gharama zinazotarajiwa kwa mujibu wa masharti ya bima husika, huku akiendelea kuhamasisha wananchi kuelewa umuhimu wa bima ikiwemo bima ya afya.Aidha, ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za umma na wadau wengine ni muhimu katika kuboresha huduma za kijamii na kuchangia maendeleo endelevu ya taifa.

Kuhusu kiasi Cha fedha kitakachokabidhiwa , amesema kiasi cha fedha taslimu kilichokuwa kimefikia Sh milioni 213.5 kimeongezeka na kufikia Sh milioni 218, huku akisema lengo ni kufikisha Sh milioni 300. Ameongeza kuwa wadau wengine wa bima wameahidi kuendelea kuchangia ili kufikia lengo hilo.

Amesema mchango huo ni sehemu ya kuendeleza utamaduni wa kusaidiana na kujibika katika jamii, huku akiwapongeza wadau wa bima kwa ushirikiano wao katika kusaidia watoto wanaopatiwa huduma katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Dkt. Jesse Kashabano, amewataka wadau kuendelea kuunga mkono Hospitali ya Benjamin Mkapa pamoja na hospitali nyingine zinazofanya jitihada za kutoa huduma kwa wananchi.

Amesema lengo la BMH ni kufikia hatua ya tiba kamili kwa wagonjwa, Ameongeza kuwa BMH inaendelea kupanua huduma za upandikizaji, ikiwemo upandikizaji wa mimba kwa kina mama, ambapo amesema wataalamu zaidi ya watano wamekwishapatiwa mafunzo katika eneo hilo na wanatarajia kuanza huduma hiyo ifikapo mwakani.Naye Mkurugenzi wa Mipango na Fedha wa BMH, CPA Ambele Msika, amesema watumishi wa hospitali hiyo wamekuwa wakiguswa na changamoto zinazowakabili wagonjwa na ndugu zao ambao wakati mwingine hukosa uwezo hata wa kupata chakula.

Amesema kutokana na hali hiyo, hospitali ilianzisha mfuko endelevu unaolenga kupata michango kutoka kwa wadau mbalimbali na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi wasio na uwezo.

CPA Msika amesema mfuko huo umepata support kutoka Mkoa, Wizara ya Afya na Serikali kwa ujumla, huku akisema Msajili wa Hazina amekuwa akitoa support kubwa katika jambo hilo.

Ameongeza kuwa kuna wazazi zaidi ya 50 wenye watoto ambao tayari wamefanyiwa uchunguzi na wataalamu na wako tayari kupatiwa huduma, lakini wanasubiri upatikanaji wa fedha na vifaa ili huduma hizo ziweze kuendelea kutolewa.